Mahakama ya Rufani Tanzania leo inaanza kupitia maombi ya mapitio ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyomrejeshea ubunge mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.
Mahakama hiyo inapitia maombi hayo ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopinga ubunge wa Lema, na kufanikiwa kumvua ubunge kabla ya Mahakama ya Rufaa kumrejeshea wadhifa wake wakitaja sababu za kuomba hukumu hiyo ipitiwe upya.
Kwa mujibu wa hati za maombi hayo zilizowasilishwa katika mahakama hiyo na makada hao kupitia wakili wao, makada hao, ambao ni wapigakura wametaja sababu sita za kuomba hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu ipitiwe upya.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa warufani, Tundu Lissu, alithibitisha kupata nakala za hati hiyo na kusema kimsingi sababu kubwa zilizotajwa na makada hao ni mbili.
Katika hati hiyo, wapigakura hao wanataja sababu ya kwanza kuwa ni hukumu hiyo kutumia sheria ya kimila ya Uingereza inayohusu kesi za uchaguzi, kinyume cha sheria ya Tanzania ya matumizi ya sheria mahakamani sura ya 358 ya sheria za nchi kifungu cha 2 (3).
Wanadai kifungu hicho kinazuia kuvuka mipaka na kutumia sheria ya Uingereza kama jambo husika limetungiwa sheria mahsusi na Bunge la Tanzania kusimamia kesi za uchaguzi.
Wapigakura hao wanadai kuwa kama ni kutumia sheria ya Uingereza, basi inayopasa kutumika ni ile ya Julai 22, 1920, ambayo kwa sasa haiko hai.
Sababu ya pili, wanadai kuwa uamuzi wa mahakama hiyo (ya Rufaa) unapingana na uamuzi mwingine uliowahi kutolewa na mahakama hiyo mwaka 1997.
Wanadai uamuzi huo wa Mahakama ya Rufaa wa mwaka 1997 ulitamka bayana kwamba, sheria itakayotumika katika kesi zinazohusu uchaguzi ni ileile ya Bunge la Tanzania.
Hivyo, wanadai Mahakama ya Rufaa imezua utata mkubwa dhidi ya sheria juu ya uamuzi wake wa Desemba 22, mwaka jana.
Sababu ya tatu, wanadai kuwa mahakama hiyo ilikosea kutamka kwamba, hakukuwa na ushahidi kwenye kumbukumbu za Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwamba, waliofungua kesi ya kupinga ubunge wa Lema hawakuwa wapigakura.
Wanadai ushahidi wa hilo ulikuwapo na kwamba, hata katika hoja 18 zilizowasilishwa na upande wa warufani (Lema), hiyo haikuwa hoja yao.
Vilevile, wanadai wanasheria wa serikali walikubali kuwa wajibu rufani ni wapigakura.
Pia wanadai wakili wa wajibu rufani alikubali hilo na hata Jaji aliyesikiliza kesi ya kupinga ubunge wa Lema alipohitaji ushahidi, alionyeshwa kadi za kupiga kura kabla ya kuwarudishia.
Sababu ya nne, wanadai Mahakama ya Rufaa ilikosea kuwekea vikwazo haki yao (wapigakura hao) ya kufungua kesi ya uchaguzi kwa kutamka kwamba: “Haki hiyo itakuwapo tu kama itakuwa imekatishwa.”
Wanadai sheria ya uchaguzi namba 111 (1) (A) haijaweka masharti na kwamba, Mahakama ya Rufaa kwa kutamka kifungu hicho, imeingiza maneno, ambayo hayamo kwenye sheria hiyo.
Wapigakura hao wanadai kuwa kazi ya mahakama ni kutafsiri na si kutunga sheria na kwamba, kazi ya kutunga sheria ni ya Bunge.
Hivyo, wanadai kitendo hicho cha mahakama kimeingilia mamlaka ya mhimili mwingine wa dola.
Sababu ya tano, wanadai kuwa mawakili hawakupata fursa ya kujibu hoja kama kifungu hicho cha maneno ya Mahakama ya Rufaa kimetungwa kiasi kwamba, kinaweza kuhitilafiana na sheria nyingine ya uchaguzi.
Wanadai kifungu hicho cha sheria ya uchaguzi kinasema: “Malalamiko ya uchaguzi yanaweza kuwasilishwa mahakamani kwa aliyepiga kura kwa mujibu wa sheria au aliyekuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi, ambao unalalamikiwa.”
“Hivyo, majaji wa Mahakama ya Rufaa wametunga sheria, wameingiza kifungu, ambacho hakipo kwenye sheria wakati mahakama haitungi sheria,” wanadai.
Sababu ya sita, wanadai imejumuishwa kwenye baadhi ya sababu zilizotajwa hapo juu, ambazo zinaifanya sheria isieleweke na mahakama isiwe na heshima, ambayo inapaswa kuwa nayo.
“Lazima tafsiri (ya sheria) iwe yenye uelekeo mmoja, isitofautiane,” wanadai.
Kwa mujibu wa taarifa za kimahakama, wapigakura hao waliwasilisha maombi yao Februari 13, mwaka huu, chini ya hati ya dharura wakitaka yasikilizwe haraka.
Desemba 21, mwaka jana Mahakama ya Rufaa ilimrejesha tena Lema bungeni baada ya kukubali rufaa yake dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge wake.
Makada hao, ambao ni Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel, walifungua kesi dhidi ya Lema katika mahakama hiyo, kupinga ushindi wake alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Walikuwa wakidai kuwa katika kampeni zake, Lema alikuwa akitumia lugha za matusi, kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Batilda Buriani.
Kufuatia kesi hiyo, Lema alivuliwa ubunge na mahakama hiyo, Aprili 5, mwaka jana, katika hukumu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo.
Jaji huyo alisikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Aloyce Mujulizi aliyekuwa amepangiwa kuisikiliza kujitoa kufuatia ombi la Lema kupitia mawakili wake, Method Kimomogoro na Lissu kuwa hakuwa na imani naye.
Hata hivyo, baadaye mwishoni mwa mwaka jana, Lema kupitia mawakili wake, alikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyomvua ubunge wake.
Hukumu iliyomrejeshea ubunge Lema ilitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wakiongozwa na Nathalia Kimaro. Wengine ni Salum Massati na Bernard Luanda
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment