WABUNGE wamepanga kuisulubu Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa kukwamisha bajeti ya Wizara ya Maji kama haitakuwa na dhamira ya kupunguza au kuondoa tatizo la maji, Tanzania Daima limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika viunga vya Bunge mjini hapa, umebaini kuwa wabunge wamechoshwa na kauli na ahadi za serikali kukabili tatizo hilo wakati hakuna dhamira ya kweli ya kuliondoa.
Wabunge wa vyama tofauti wanaotoka mkoa au wilaya moja zenye shida ya maji, wameunganisha nguvu kutaka kukwamisha bajeti hiyo.
Wizara hiyo kupitia kwa Waziri wake, Profesa Jumanne Maghembe inatarajia kusoma mwelekeo wa bajeti yake leo na itajadiliwa kwa siku mbili.
Katika mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyopitishwa wiki iliyopita, wabunge wengi akiwemo wa Same Mashariki, Anna Kilango (CCM) walichangia kwa hisia kali suala la maji.
Mbunge wa Nkasi, Ally Kesi (CCM) ambaye mwaka jana alipata upendeleo maalumu baada ya kutishia kwamba angewaleta wanawake wa jimbo lake bungeni, alisema maji ni kero namba moja kwa sasa nchini.
Mbali ya kujadili tatizo hilo kwa hisia kali bungeni, nje ya ukumbi wa Bunge mjadala wa maji umetawala.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa hofu ya wabunge wa CCM ni kwamba endapo serikali haitatenga fedha za kutosha kukabili kero hiyo, wanaweza kupoteza nafasi zao mwaka 2015.
“Kila mwaka serikali inakuja na lugha nzuri kueleza namna ya kutatua kero hiyo, lakini mwisho wa mwaka wa bajeti hakuna kitu. Safari hii patachimbika,” alisema mbunge mmoja wa mikoa ya kusini.
Baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam waliliambia Tanzania Daima kuwa safari hii moto utawaka kwani serikali ilisema imetenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na kero hiyo jijini humo na kwamba lingekuwa historia.
Wabunge kadhaa waliozungumza na gazeti hili na kuomba majina yao yahifadhiwe kwa hofu ya kunyimwa nafasi ya kuchangia, walisema kwa nyakati tofauti kwamba wasipotengewa fedha kwa ajili ya miradi ya maji patachimbika.
Wapo wanaokumbuka hoja binafsi ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) kulitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza kero hiyo na kuja na mapendekezo ambayo yangeisaidia serikali kukabiliana nayo.
Hata hivyo, hoja hiyo iliyozimwa kishabiki na wabunge wa CCM, leo inaonekana kuwa na maana zaidi na kumpa sifa Mnyika.
Wakati wabunge wakipanga kukwamisha bajeti hiyo, serikali kwa upande wake inahaha kupata sh bilioni 200 zaidi kuongeza kwenye miradi ya maji nchini.
Hatua hiyo ya serikali imetokana na ushauri wa Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Kamati hiyo imeelezwa kuifumua bajeti yote na kuisuka upya kuhakikisha kila jimbo linapata mgawo wa fedha za miradi ya maji.
“Kamati ya Bajeti imefanya kazi kubwa sana, maana imefumua bajeti yote ya awali na kuisuka upya. Itakaposomwa, kila mbunge ataifurahia,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Kuongezeka kwa fedha hizo kutafanya bajeti ya wizara hiyo kwa mara ya kwanza kutengewa fedha nyingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Katika mwaka wa fedha wa 2012/13, wizara hiyo iliomba na kuidhinishiwa sh bilioni 568.8.
Licha ya sekta ya maji kuwa moja ya vipaumbele vya serikali, kiasi hicho kilikuwa pungufu kulinganisha na sh bilioni 621.6 za mwaka 2011/12.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge walimtuhumu vikali Waziri Maghembe kuwa hatekelezi wajibu wake.
Kwa mujibu wa sera ya maji ya mwaka 2002, kila mwananchi anatakiwa apate maji ndani ya umbali wa mita 400 kutoka mahali anapoishi.
Hata hivyo, maeneo mengi nchini hasa vijijini, wananchi hulazimika wakati mwingine kutembea zaidi ya kilomita 20 kutafuta maji au kutumia saa 12 kuyasubiri.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment