Friday 26 April 2013

Wabunge hivi mnaridhika na Khanga Moko?





Khadija Kalil

 AHLANWASHLAN mpenzi msomaji wa safu ya Busati la Wikiendi, inayokujia kila siku kama ya leo.
Au baada ya salaam, msomaji wangu ikiwa waheshimiwa wabunge la Jamhuri ya Muungano wanaendelea na mikutano yao huko Dodoma, wakizungumzia mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa nchi, nina ujumbe kwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Ikiwa ndiyo wizara mama ya masuala yanayohusu michezo, utamaduni na vijana, nawaomba kwa mara nyingine tena, watupie macho makundi ya sanaa yanayovunja maadili ya utamaduni wa Mtanzania.
Uvunjwaji wa maadili unaofanywa na makundi hayo, hivi sasa unazidi kuota mizizi na kunawiri kila kukicha, huku wahusika wakionekana kufumbia macho licha ya vilio vingi kutaka hatua zichukuliwe.
Makundi kama Khanga Moko ‘Laki Si Pesa’, Kitu K na mengine yanazidi kujizolea ‘sifa’ kuvunja maadili ya Kitanzania katika maonesho yao mbalimbali.
Waheshimiwa wetu mnapokutana mjengoni, burudani nyingi tunatarajia zitaletwa huko, lakini kuna makundi mengine mnapaswa kuyakemea kwa nguvu zote na siyo kwa kuiachia wizara pekee.

Kundi hili la Khanga Moko, limekithiri sasa na hii yote sijui ni kwa sababu linamilikiwa na mnene mmoja au kuna ubia, hatufahamu.
Inashangaza sana, kundi hili kuendelea kupewa vibali vya kufanya maonesho yake katika sehemu mbalimbali za nchi.
Awali, lilianzia katika kitongoji cha Mwananyamala na baadaye likasambaa jiji la Dar es Salaam na sasa limeamua kwenda mbali zaidi kwa kufanya maonesho yake mikoani, ambako walikuwa hawajaathiriwa na minenguo ya kundi hili.
Najua wapo baadhi ya watu watashangaa ninavyosema kuathiri, kusema kweli, kundi hili linaathiri sana watu wazima na hata wenye miaka chini ya 18 pia.
Kwanza, hawafurahishi zaidi ya kumchefua mtazamaji, kwani hata wao wanaokwenda kutazama, hujikuta wakioneana aibu kutazama, sasa raha hapo iko wapi?
Heshima na utu wa mwanamke, vimekuwa vikidhalilishwa huku wenye dhamana wakikaa kimya bila ya kuchukua hatua ya kulifuta kundi hilo ama vinginevyo.
Najua katika hili kwamba wapo baadhi ya watu watakaoona nahatarisha ajira zao, lakini ukweli ndiyo huo, kundi hili halitufai sisi watu wazima, vijana na hata watoto pia.
Ni wajibu wa serikali, kulifungia kundi la Khanga Moko na pia kupiga marufuku vikundi vichanga vinavyochipukia huku vikinengua katika miondoko hiyo hiyo ya Khanga Moko.
Mwaka jana Bungeni, wabunge walijaribu kulipapasa kidogo tu suala hili, lakini bado wamekuwa vibogoyo na kushindwa kuwang’ata watu wachache ambao wamekuwa wakiharibu utamaduni wa Mtanzania.
Kama hiyo haitoshi, wapo wabunge wanawake, lakini kama vile wanabariki jambo hili.
Mtetezi wa kwanza wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe; hivi mtavumilia kudhalilishwa kwa mwanamke hadi lini?
Wabunge wanawake, hebu simameni imara na kuweka msisitizo wa kulishughulikia kundi hili, ikiwezekana hata kuzuia shilingi katika wizara husika, labda serikali itawasikia.
Binafsi yangu nimekuwa naandika sana habari za kundi hili tangu lilipoanzishwa hadi sasa, sijachoka, japokuwa najua kwamba wapo wanaonichukia au watakaoendelea kunichukia kwa kuwa nimekuwa nakutana nao mitaani, lakini sitakoma kukemea hali hii hadi kieleweke.
Ikumbukwe kwamba hii ni aibu hata kwa nchi za jirani, pindi watakapoona ngoma hizi, kwani watajua tuna utamaduni wa kishenzi na usiofaa katika jamii.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki mama wa Kitanzania.
                                                  
                     chanzo:daima                                

No comments:

Post a Comment