Thursday, 4 April 2013

Walipwa Sh6.9 bilioni kupisha bomba la gesi

Serikali imesema wananchi 3,092 wamelipwa jumla ya Sh 6.9 bilioni fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, ambalo ujenzi wake unatarajiwa kugharimu Sh9.3 bilioni. Taarifa iliyopatikana kutoka kwenye kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka 2013/14, iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilieleza kuwa fedha hizo ni za ndani, ambazo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa km 532 (Mtwara-Dar es Salaam na kipenyo cha inchi 36 yameanza, ambapo jiwe la msingi liliwekwa tangu Novemba mwaka 2012. “Mabomba yameshaanza kusambazwa katika njia litakakopita bomba hilo, aidha fidia ya ardhi kupisha ujenzi imekamilika, ambapo wanakijiji wapatao 3,092 wamelipwa,fidia ni Sh6 857,746,020,” ilielezwa katika taarifa hiyo. Utekelezaji wa mradi wa mtambo wa kufua umeme Kinyerezi (MW 240), umekwama kutokana na kuchelewa kwa majadiliano baina ya Serikali na benki ya kimataifa ya Japan. Imeelezwa kuwa mradi huo ambao unagharimiwa kwa mkopo kutoka katika benki hiyo ya Japan ambao watachangia asilimia 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini ambayo inachangia kwa asilimia 15. “Ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani 432,137,936, haujaanza kutokana na kuchelewa kwa majadiliano ya mkopo baina ya Serikali na Japan na kigezo cha kufanya uhakiki wa mradi kilichowekwa na Benki ya Afrika,” ilielezwa katika taarifa hiyo. Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ulizua mgogoro wa aina yake mwaka jana kati ya wananchi na Serikali, baada ya wananchi wa mkoa huo waliungana na kuweka itikadi zao pembeni ili kuupinga. chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment