Monday 10 June 2013

Diamond, Jaydee wasanii bora 2013


Wasanii Diamond na Lady Jaydee walitwaa tuzo za wasanii bora wa kiume na wa kike wa mwaka katika tamasha la Kilimajaro Music Awards juzi usiku, lakini ilikuwa ni bendi ya muziki wa dansi ya Mashujaa 'Wana Kibega' iliyozoa tuzo tano kati ya 37 zilizotolewa kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Nyota wa muziki wa kizazi kipya, Kala Jeremiah na Ommy Dimpoz walifuatia nyuma ya bendi hiyo wakizua tuzo tatu kila mmoja.

Wimbo wa 'Risasi Kidole' ndiyo ulioibeba bendi ya Mashujaa katika tuzo hizo ukishinda tuzo ya wimbo bora wa bendi wa mwaka, huku rais wa bendi hiyo na muimbaji nyota Chalz Baba akishinda tuzo ya mtunzi bora wa bendi wa mwaka jana huku tuzo ya tatu ni bendi hiyo kutangazwa kuwa bendi bora iliyofanya vyema mwaka jana.

Rapa wa bendi hiyo, Saulo Ferguson alishinda tuzo ya rapa bora na huku tuzo ya tano ikienda Chalz Baba akiwa msanii bora wa kiume wa bendi akiwaangusha, Dogo Rama na Greyson Semsekwa wa African Stars 'Twanga Pepeta' na Jose Mara na Khalid Chokoraa kutoka bendi ya Mapacha Watatu.

Chalz baada ya kupokea tuzo hizo alisema kuwa huo ni mwanzo na mambo matamu zaidi yanakuja hivi karibuni ambapo ameshayarisha vibao vipya viwili viitwavuo 'Usiidharau Sifuri' na 'Ushamba Mzigo'.


Mwimbaji huyo wa zamani wa Twanga Pepeta hakusahau kumtaja marehemu Abuu Semhando kuwa ni mmoja wa watu waliomfanya yeye afike alipo na pia akasema kwamba ushirikiano wa wanamuziki na viongozi wa bendi ya Mashujaa ndiyo uliowapa mafanikio hayo.

"Kufa na kiu baharini ni uzembe," Chalz alisema baada ya kuchukua tuzo ya tano akisindikizwa pia na meneja wa bendi, Martin Sospeter na rapa Ferguson.

Kala Jeremiah, aliyeibuliwa na shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search, alipata tuzo ya wimbo bora wa mwaka (Dear God), tuzo ya mtunzi bora wa Hip Hop na ya msanii bora wa mashairi ya muziki huo ambapo baada ya kupata tuzo ya tatu alianza kwa kumshukuru Mungu kwa mafanikio hayo ambayo hakuwahi kuyapata tangu aanze muziki huku pia akimshukuru mkurugenzi wa BSS, Madame Ritha, kwa kukuza kipaji chake.

Video iliyopondwa kwenye mitandao ya kijamii ya wimbo 'Me and You' ya Ommy Dimpoz ilishinda tuzo ya video bora ya mwaka, huku pia wimbo huo aliomshirikisha Vanessa Mdee ukimpa tuzo ya wimbo bora wa kushirikiana na wimbo bora wa mwaka.

Ommy Dimpoz kabla ya kupokea tuzo yake ya tatu aliwaomba wamiliki wa makampuni na taasisi mbalimbali kuwatumia wasanii katika kutangaza bidhaa zao na kuacha kutumia wanasoka pekee.
"Tumechoka kuzika wasanii wenye majina makubwa wakiwa masikini, tutumieni katika promosheni kama mabalozi," aliongeza msanii huyo.

Katika tuzo hizo zinazodhaminiwa na kampuni ya bia nchini (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro, Diamond ambaye hakuwapo ukumbini alichukua tuzo nyingine ya pili ya msanii bora wa kiume wa bongo flava wakati Recho kutoka THT aliitwaa tuzo kama hiyo kwa upande wa wasanii wa kike.

Malkia wa mipasho nchini, Khadija Kopa, ambaye hakuwapo ukumbini baada ya iliyopita kufiwa na mumewe, alishinda tuzo ya wimbo bora wa taarab (Mjini Chuo Kikuu) wakati Isha Mashauzi wa Mashauzi Classic aliibuka kidedea kwa kutwaa tuzo ya msanii bora wa kike wa muziki wa taarab na kwa wanaume, Mzee Yusuph aliwashinda, Ahmed Mgeni na Hashim Said.

Tuzo ya msanii bora wa kike wa bendi ilichukuliwa na Luiza Mbutu wa Twanga Pepeta, Thabit Abdul alipata tuzo ya mtunzi bora wa mashairi ya taarab wakati Ben Pol alitwaa tuzo ya mtunzi bora wa mashairi ya bongo flava huku Man Water akiibuka mtayarishaji bora wa muziki wa mwaka akiwaangusha wenzake sita waliokuwa wakiiwania tuzo hiyo, Bob Junior, C9, Ima The Boy, Maneke, Marco Chali na Mensen Selecta.

Enrico alishinda tuzo ya mtayarishaji bora wa wimbo wa taarab huku Selekta akitwaa tuzo ya mtayarishaji chipukizi wa muziki wa kizazi kipya na Amoroso aking'aa kwa upande wa mtayarishaji bora wa wimbo wa bendi kwa mwaka jana.

Kibao cha 'Chocheeni Kuni' cha Mrisho Mpoto a.k.a Mjomba kilitwaa tuzo ya wimbo bora wa asili, wakati wimbo 'Kilimanjaro' wa kundi Warriors From the East kutoka Arusha ukishinda tuzo ya wimbo bora wa reggae na tuzo ya wimbo bora wa muziki wa ragga (dance hall) ilikwenda kwa Predator (Dabo).

Amini alishinda tuzo ya wimbo bora wa zouk (Ni Wewe) na kundi la Jahazi lilitangazwa kuwa kundi bora la muziki wa taarab wakati Jambo Squad walichukua tuzo ya kundi bora la muziki wa Hip Hop huku Mganda Jose Chameleone akitwaa tuzo ya wimbo bora wa Afrika Mashariki (Valu Valu).

Tuzo ya heshima ilikwenda kwa bendi ya Kilimanjaro 'Wana Njenje' iliyoanzishwa mwaka 1970 ikianzia mkoani Tanga huku tuzo ya heshima kwa msanii mmoja mmoja ilikwenda kwa marehemu Salum Abdallah Yazidu kutoka Morogoro aliyeimba kibao cha 'Shemeji Shemeji' na kufanya kazi katika bendi mbalimbali ikiwamo ya Dar es Salaam Jazz.

Katika kunogesha tamasha hilo wasanii mbalimbali walitumbuiza lakini mashabiki waliohudhuria walionekana kupagawa zaidi na Fresh Jumbe aliyeimba kibao cha 'Zeze' cha TID, Zahir Ally Zoro aliyeimba wimbo wa Mr Nice uitwao 'Kikulacho' na Jose Mara na Vumilia wa THT walioimba kibao cha 'Gere' cha Wana Njenje ambacho kwa kawaida huimbwa na Waziri Ally na Nyota Waziri.

Wanamuziki wengine waliotoa burudani katika usiku huo ni pamoja na Lina, Amini, Saida Karoli, Snura (Majanga), Barnaba, Ben Pol, Madee, Mabeste na Godzila ambaye alianza kwa kuimba kibao cha 'Getho Langu' kilichoimbwa na marehemu, Albert Mangweha 'Ngwair' aliyefariki dunia nchini Afrika Kusini hivi karibuni na kuzikwa kwao Kihonda, mkoani Morogoro.

Mtangazaji wa kituo cha radio na televisheni cha East Africa (EATV), Zembwela, ambaye alikuwa MC wa shughuli hiyo alikuwa ni kivutio kutokana maneno yake ya uchekeshaji aliyokuwa anazungumza katika usiku huo.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment