Saturday, 15 June 2013

Lady Jaydee na Mwana FA, weledi wenu utadhihirika leo


SALAAM aleikum msomaji wa Safu ya Busati. Leo usiku kwa wale mashabiki wa muziki, watajivinjari katika kumbi za Makumbusho kwa mwana Hip Hop nguli Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ na Nyumbani Lounge ambako atakuwepo Mwanadada nguli, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’.
Wakati Mwana FA akiwa katika onesho lake la ‘The Finest’ anaposherehekea miaka 18 tangu alipoanza muziki, huku Lady Jaydee akifanya sherehe ya miaka 13 tangu alipoanza muziki pia.
Ukiangalia kwa makini, matamasha yote haya yanaonekana kila mmoja akifanya kitu kwa sababu ya kazi yake, hapo nawapa hongera sana kwa hapo walipofikia.
Hivyo basi, sisi wadau ambao tutabahatika kufika katika maonesho haya, tunatarajia kujifunza kitu, kwani kila mmoja tunatarajia ataonesha jinsi alivyoiva katika ‘game’, hivyo weledi wenu utadhihirika leo.

Tukiangalia hivi sasa, wasanii wengi wanaibuka kila uchao, nao bila shaka watakuja katika maonesho haya, hivyo yatumike kama sehemu ya darasa kwa wasanii wetu wachanga.
Kwa maoni ya safu hii, naona kwamba kuna kitu kikubwa cha kujifunza katika matamasha haya, hasa kwa wale wasanii wenye njozi za siku moja kuwa kama Mwana FA au kama Lady Jaydee.
Katika onesho la Lady Jaydee, kutakuwa na kiingilio cha sh 50,000 pamoja na chakula cha usiku huku wakisindikizwa na bendi ya Machozi anayoimiliki msanii huyo.
Onesho la Lady Jaydee limedhaminiwa na Michuzi Blog na East Africa TV (EATV).
Aidha pia Jaydee atazindua video yake ya kibao ‘Nothing But The Truth’ kikiwemo kibao chake cha ‘Joto Hasira’, huku nguli wa dansi, Komandoo Hamza Kalala akisindikiza tamasha hilo.
Kwa upande wa Mwana FA, amedumu kwa miaka 18 sasa katika ‘game’; bila shaka atafanya onesho la kiutu uzima zaidi, kwa sababu moja kubwa kwamba, laiti kama angelikuwa ni kijana, pindi anapotimiza umri wa miaka 18, jamii inayomzunguka pamoja na familia humwesabu kuwa ni mtu mzima na hata jambo lolote atakalolifanya, anakuwa amelifanya kwa ridhaa yake huku akitambua lolote analolitenda kwa ujumla.
Mwisho, napenda kuona sanaa ya Bongo ikipanda na jukumu hili liko mikononi mwenu ninyi wasanii, hivyo kuweni makini katika kila hatua ya kazi zenu mnazozifanya ili ziweze kuleta mrejesho wenye tija katika tasnia ya muziki na si vinginevyo.
Nawatakia sherehe njema, bila kusahau kuwapongeza kwa dhati inayotoka katika uvungu wa Safu ya Busati, kwa hapo mlipofika, kwani siyo padogo na mafanikio yote mliyoyapata kwa kupitia muziki na kuwatakia Mungu awazidishie umri na nguvu, pamoja na ari ya kuendeleza muziki wa hapa nchini.
Vilevile kwa kumalizia tu, wasanii wote hawa kama ilivyo kwa Mwana FA ambaye anasema anakumbuka tangu siku yake ya kwanza alipopanda jukwaani na kuahidi atatoa masimulizi yake katika mtindo wa kiburudani, ili jamii iweze kung’amua nani aliyechangia kumfikisha hapo alipo sasa.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment