Sunday, 23 June 2013

Mangwea ameniacha kwenye mikono salama

“KIFO cha Albert Mangwea ‘Ngweair’ kimewagusa wengi, lakini kwangu ni zaidi kwa sababu alikuwa ni zaidi ya ndugu. Niliamini angeweza kusimamia kazi zangu zote.
Lakini haikuwa hivyo badala yake alishuhudia kazi zangu mbili pekee. Ila nashukuru ameniacha katika mikono salama ya wasanii kama Dark Master na Jeezy Mabovu walioniahidi kunisaidia katika safari yangu ya kimuziki.” Haya ni maneno ya Rodrick Kasongwa ‘Mjukuu wa Chamber’ au ‘Mtzee’.
Akizungumzia maneno ya mwisho kuzungumza na marehemu Ngweair kwenye simu siku tatu kabla ya kifo nchini Afrika Kusini, anasema alimweleza kwamba huko kuna suruali za jeans ambazo hazichuji hata zikifuliwa kwa maji ya chumvi.
“Dogo huku (Afrika Kusini) kuna suruali kali za jeans ambazo hazichuji hata ukifulia maji ya chumvi, nakuahidi kukuletea tatu,” anasema R kwenye mahojiano na Tanzania Daima mapema wiki hii.

R anayetamba kwa sasa na wimbo ‘Nipeni nafasi’ ambao ameutengeneza kwenye studio za Racers za Morogoro chini ya mtayarishaji GQ, anasema kama isingekuwa Ngweair hata yeye  asingekuwa msanii.
Akielezea alivyokutana na Ngweair, anasema mwaka 2005 wakati huo aliachia kazi yake iliyokwenda kwa jina la ‘Usije Ukaringa’ akiwa amemshirikisha Bize Mtzee waliyoifanya katika studio za Bad Namba.
Ngoma hiyo haikutamba kama alivyokuwa amefikiria, hali iliyomfanya akate tamaa, lakini baada ya kukutana na Ngweair nyumbani kwao Kihonda, Morogoro wanapoishi jirani alimpatia moyo wa kuendelea na kazi hiyo.
Anasema Ngweair alimuunganisha na wasanii wengine wa kundi la Chamber Squad kama vile Dark Master, Jeezy Mabovu na Jordan, ambapo aliwasihi kujiunga na kundi hilo.
Lakini anasema Dark Master ambaye alikuwa kiongozi wa kundi hilo, alimkatalia na kumwambia atakuwa mwanafamilia akiwa kama mjukuu kwa sababu kundi hilo lilianzia shule.
“Hapo ndipo akanipatia jina la mjukuu wa Chamber Squad au mjukuu wa Kihonda,” anasema na kuongeza kwamba kuanzia hapo alianza kujifua zaidi kwa ajili ya kuachia ngoma kali zaidi.
Anasema mwaka juzi walipanga kufanya kazi na Ngweair iliyokuwa ikienda kwa jina la ‘Plate Number’, ikiwa chini ya mtayarishaji Nabii the Cord, lakini malengo hayo hayakufanikiwa kutokana na mtayarishaji huyo kufariki dunia wiki ambayo Ngweair alitarajiwa kuingiza sauti.
Ngweair akashauri ngoma hiyo wairudie mwaka huu kwa mtayarishaji Corner Beats wa Studio za HM Studio lakini wakati tunapanga kurudia ndipo katika wiki hiyo Ngweair akaelekea Afrika Kusini ambako mauti yakamkuta.
Anasema kuwa baada ya kazi yake ya ‘Nipe Nafasi’ kutamba hivi sasa Diwani wa Boko, maarufu kama Maji Safi akajitolea kumsimamia kazi zake kwa kumlipia studio na kuzitangaza.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa albamu, Pick R, anasema hatatengeneza albamu bali atakuwa akitoa ngoma moja moja kali ambazo atakuwa akitumia kupigia shoo.
Akielezea sababu za kutotoa albamu alisema inatokana na kukwepa kutumia fedha nyingi kuitengeneza huku akiishia kuingiza kiasi kidogo kama wafanyavyo wasanii wengi nchini. 
Maoni yake
Anasema kwamba anakerwa na wale wote wanaomzungumzia vibaya Ngweair kwa kusema alikufa maskini bila ya kujua kuwa wale waliokuwa wakimsimamia mwanzo ndio hao wanaowasimamia wao.
Alipotoka
Msanii huyo aliyezaliwa mwaka 1987 Mkoani Morogoro akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne.
Mwaka 2001 baada ya kuhitimu Darasa la Saba katika Shule ya Msingi huko Kihonda, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Tech Fort ya Ikara, Kilombero aliposoma kwa miaka miwili.
Anasema akiwa hapo, ndipo alianza sanaa ya uimbaji wakati huo akiimba kwenye sherehe za kumaliza kuwakaribisha kidato cha kwanza na sherehe za kumaliza kidato cha nne.
“Mwaka 2003, nilihamia katika Shule ya Sekondari ya Kigurunyembe, Morogoro ambako alihitimu kidato cha nne mwaka 2004.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment