Sunday, 23 June 2013

Obama aje lakini ajibu haya, pia tusione aibu, tuulize hiki kitendawili kiteguliwe.


KATIKA safu hii wiki iliyopita niliponda sana ziara ya Obama, niliandika kumuarifu kuwa sisi watanzania hatudanganyiki kwa kauli iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini kusema kuwa kati ya vitu vilivyomfanya Obama kutembelea Tanzania ni kwa sababu Tanzania kuna utawala bora.
Ubalozi wa Marekani nchini, licha ya kujionea mabomu yanayolipuka kuua, kujeruhi na kutesa Watanzania, licha ya vitendo vya kikatili vinavyoendeshwa na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Mkoa wa Mtwara, licha ya mauaji yaliyofanywa na polisi sehemu mbalimbali nchini, bado umeona utawala huo ni wa kuvutia, unaopaswa kupewa hadhi ya ziara ya Rais wa Marekani.
Shukrani zangu zimwendee mwandishi wa Kimarekani, Dana Milbank, mwandishi wa gazeti la Washington Post, japo hatufahamiani aliendana sana na mawazo yangu kuwa ziara ya Obama nchini ni kuja kuhalalisha biashara ya kusafirisha watu, huku akimlaumu mwanadiplomasia wa Tanzania aliyehukumiwa kulipa dola za Marekani milioni moja kwa kitendo cha kudhalilisha mtumishi wake.
Lakini licha ya kuhukumiwa kulipa alitoroka Marekani na kwa mujibu wa gazeti hilo la Washington Post, mwanadiplomasia huyo alikuja kuteuliwa kuwa mshauri wa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Dana Milbank anahoji itakuwaje Obama akutane na mtu ambaye si muadilifu? Na anayelindwa na Ikulu ya Tanzania kutotekeleza amri halali ya mahakama kwa makosa aliyotenda.
Tanzania tumevuka rekodi, na sasa tunaenda kinyume nyume, waliowachafu tunasema wasafi, waliostaafu tunawaongezea muda wa kuongoza hadi wazeeke hata kama wana tuhuma nzito, waliopaswa kushushwa vyeo tunawapandisha.

Katika hili ningekuwa Jaji Amiri Manento ningejiuzulu ili kulinda heshima, maana ushauri waliotoa kuhusu Michael Kamuhanda, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ulipuuzwa mchana kweupe, akapandishwa cheo.
Jaji na jopo lake wanaonekana hewa tu mbele ya jamii kwa ushauri waliotoa na Kamuhanda ameongezewa cheo na kuhamia makao makuu anakula bata. Manento na wenzake wabaki na makabrasha yao, ‘watajiju.’
Watanzania tumeongozwa na Bunge letu miaka mingi, likiwa limesheni wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wengi kwa idadi yao, wanaopenda kujifungia katika ukumbi wa Msekwa ili wakitoka wakubali bila kuhoji, hata mambo ambayo yapo wazi kabisa. Kifupi ukumbi wa Msekwa ni eneo lililotumika muda mrefu kubariki maumivu kwa Watanzania.
 Bunge letu na wabunge wetu wamechangia tuongozwe kijinga, wabunge wetu wamekubali mambo yasiyowezekana, hawakuhoji kwa ukweli, hawakuhoji kwa akili, hujifurahisha kwa kupiga makofi na kufuata kanuni za Bunge hata nyingine zinazohalalisha uharamia.
Huu ndio utawala ambao Obama ameusifu kwa kuwa anajua hata akiingia mikataba ya gesi na petroli kama anajua wabunge wetu hawatahoji, wataingia ukumbi wa Msekwa, wakitoka kule watalinda heshima ya Chama Cha Mapinduzi ili gesi, madini, ardhi yetu na petroli vichukuliwe vema na Marekani. Mti ukue kwetu, kivuli Marekani.
Tumelazimika kukubali mambo fulani yasiyovutia nchini kwa sababu ya kukosa wabunge makini, tumepewa maelezo ya kitoto kuhusu msiba wa aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Balali.
Ingefaa kama Obama naye si kama wabunge wa CCM basi angalau afunguke ajibu kiu ya Watanzania kuhusu gavana wao huyo wa zamani wa Benki Kuu.  
Kuna maswali ambayo wabunge waliyaacha wakaingiza taifa kwenye utata. Balali alikuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), taasisi nyeti kabisa ya serikali.
Tunakataza wabunge kuwa na uraia wa nchi mbili, wabunge waliruhusu vipi gavana kuwa na uraia wa nchi nyingine?
Tuliambiwa kuwa Balali amefia Marekani, suala hili limekuwa na sintofahamu kubwa, Obama, yeye mwenyewe, au ubalozi wake utuambie je, kweli Balali amefariki na kuzikwa nchini Marekani? Kama kweli alifariki kwanini Marekani haikuruhusu mazishi haya kuhudhuriwa na Watanzania?
Hivi wabunge wetu ni wangapi wanajua idadi ya wabunge waliowakilisha Watanzania kwenye msiba wa Balali? Wabunge wangapi walihoji kuhusu msiba wa Balali kuhudhuriwa kwa kadi za mwaliko?
Je, ni utamaduni wetu? Wabunge wetu hawakujua haya, wamewaficha Watanzania. Obama au Ubalozi wa Marekani wapo tayari kutuwekea hadharani majina ya Watanzania waliohudhuria msiba wa Balali?
Baada ya kutangazwa msiba wa Balali, wananchi wa Kitanzania waliolelewa kwa maadili ya Kiafrika walikwenda kuhani msiba katika nyumba yake jijini Dar es Salaam, lakini walipokusanyika walitimuliwa na askari wa serikali ya Tanzania kama walivyotimuliwa waombolezaji wa Soweto, Arusha juzi. 
Obama na Ubalozi wa Marekani watuambie hili suala linakubalika kwao? Ilikuwaje waombolezaji waliojitolea kwa nia nzuri kwa mila na desturi za Kiafrika wasiruhusiwe hata kukusanyika pamoja na wafiwa ambao walikuwa majirani na marehemu kabla ya kupatwa na kile kilichozua maswali?
Hili suala limezidisha shaka kama kweli Balali alifariki dunia, Obama na ubalozi wao watuambie ukweli kuhusu hili, vinginevyo na wao ni kama watawala wetu wanaopandisha vyeo wauaji, wanaotawanya waombolezaji, na kuchagua wanaodhalilisha kina dada kuwa washauri wa Ikulu ya Tanzania, kama alivyofanya mwanadiplomasia wa Kitanzania nchini Marekani.
Obama licha ya kuwa Mmarekani, anafahamu vema mila na desturi za Kiafrika, je, yaliyojiri kwenye msiba wa Balali yalifuata utaratibu gani? Kama si utamaduni wetu je, ni utamaduni wa wapi?
Kwanini utaratibu huu ulibuniwa kwa gavana huyu tu aliyeongoza taasisi nyeti nchini? Aligua na kufia nje ya nchi kama tulivyoarifiwa, ni sawa. Serikali iligharamia mazishi hayo? Kwanini ilishindwa kumrejesha nyumbani? Kwa mabomu ya Arusha tu sh milioni 100 za haraka zimetolewa, je, kiasi kama  hicho kilishindikana kutolewa kusafirisha msiba wa Obama hadi Dar es Salaam?
Kama serikali yetu ilishindwa, kwanini haikuomba msaada kwa Marekani yenyewe isafirishe huo mwili?
 Kupitia Ubalozi wa Marekani, Obama atuambie serikali ilitoa kipaumbele kwa viongozi wangapi nchini kuhudhuria hata kama ni kwa kadi za mwaliko waliopita ubalozini na kuandika katika kitabu hicho kuwa walikuwa wanakwenda kuhani msiba?
Vipi hata mkuu wa mkoa wake alikotokea au mkuu wa wilaya yake? Kama hawakuhudhuria walikosa pesa au walinyimwa kadi za mwaliko kuhudhuria?
Yawezekana kuwa hawa wote hawakuhudhuria, je, wabunge wamewahi kuiuliza serikali ilitoa kipaumbele kwa kina nani kuhudhuria msiba huo na ilitumia vigezo gani?
Mbona kwenye misiba siku hizi tofauti za kisiasa zinawekwa pembeni, kuna viongozi wangapi wa CCM walihudhuria au hata wa vyama vya upinzani?
Wabunge wamekuwa kimya wakati wanaambiwa marehemu alihusika moja kwa moja kulifanya taifa letu liwe jinsi lilivyo sasa.
Wabunge wamekaa kimya kwa suala hilo hadi sasa. Yawezekana serikali ilikosa pesa kuwasafirisha watu hao kwenda msibani, lakini vipi kule msibani hawakurekodi hata mkanda wa video ili wawaoneshe wananchi wao kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) inayoendeshwa kwa kodi za wananchi?
Inawezekana vipi msiba wa Gavana wa Benki Kuu ukakosa hata mtu wa kurekodi matukio? Au basi potelea mbali wa kurekodi angekuwa wa bei kubwa, je, mpiga picha wa Ikulu, au wa serikali mbona asioneshe hata picha ya mazishi katika gazeti la serikali linalojihusisha zaidi na siasa za chama au ufujaji wa sadaka za kanisani na mienendo ya wachungaji wa makanisa? Haya yote wabunge wameuliza? Au wapo tu wanashabikia serikali kuwaogopa wazee wa Loliondo na Mtwara?
Swali kwa wabunge popote mnaposafiri kwenda Dodoma, tujibuni mnakwenda huko kwa ajili yetu au kwa ajili yenu? Je, tuendelee kuwaamini kwa kutouliza maswali ya maana kwa masilahi ya taifa?
Tumekaa gizani muda mwingi, niwaombe Watanzania Obama akija tusione aibu, tuulize hiki 
kitendawili kiteguliwe.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment