Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), ametaka Serikali kuhakikisha wajawazito wanaojifungua gerezani watoto wao wasikae ndani ya gereza.
Akiuliza swali bungeni jana, Nyerere alisema watoto hao siyo wafungwa hivyo kuwaweka gereza ni ukiukaji wa haki za watoto.
“Lini Serikali itaachana na tabia hiyo ya kuwaunganisha watoto na wafungwa, kwa kuwa hali hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu na ni jambo la aibu?” Alihoji Nyerere.
Katika swali la msingi, Leticia alitaka kujua Serikali itapoondoa msongamano magerezani, hasa Gereza la Ngudu ambalo limezidiwa na idadi kubwa kuliko uwezo wake, hivyo kufanya wafungwa na mahabusu kuishi kwa tabu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima alisema wajawazito wanaoingia gerezani ni wahalifu na kwamba, kuna mazingira ambayo hayaepukiki kutowapeleka gerezani wajawazito hao. Alisema Serikali ipo kwenye utaratibu wa kuwa na magereza ya watoto, kuwaepusha kuchanganywa na watu wazima.
Awali, akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Silima alisema Serikali inatambua matatizo ya msongamano wa wafungwa nchini, hususan Gereza la Ngudu, wilayani Kwimba, Mkoa Shinyanga.
“Serikali imekuwa ikiyatatua kwa awamu kwa kuyafanyia ukarabati magereza yaliyopo, kukamilisha na kujenga mapya wilaya ambazo hazina magereza, lengo ni kuongeza nafasi za kuhifadhi wafungwa magerezani,” alisema.
Kuhusu ucheleweshaji upelelezi, Silima alisema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imeunda Kikosi Kazi kushughulikia msongamano magerezani, watatoa fursa ya watu kuishi kulingana na idadi ya magereza.
Alisema kikosi hicho kitabainisha vyanzo na sababu za msongamano na kutoa mapendekezo yake kwa Serikali juu ya hatua za kuchukua.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment