Monday 3 June 2013

Sheikh Ponda ataka tume kushughulikia madai ya Waislamu

Katibu wa Taasisi za Kiisilamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda ameiomba serikali kuunda tume kwa lengo la  kushughulikia madai ya Waisilamu nchini ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara dhidi yao.

Ponda aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam jana katika kongamano la amani la Waislamu lililofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambalo lilishirikisha Waisilamu kutoka mikoa mbalimbali.

Aidha, alisema serikali isipofanya hivyo Waislamu wataendelea kudai haki zao kupitia mihadhara, makongamano, maandamano na wataandaa maandamano makubwa nchi nzima yatakayofanyika usiku na mchana.

“Tunaiomba serikali iunde tume kushughulikia madai yetu sisi Waislamu tofauti na hivyo tutadai haki zetu kupitia maandamano makubwa ambayo yatafanyika mchana na usiku hadi kieleweke,” alisema Ponda.

Akizungumzia Katiba mpya, Ponda alisisitiza kuwa maoni ya Waislamu yasipoingizwa katika katiba patachimbika bila kufafanua kitakachotokea.


Kwa upande wake, Sheikh Kondo Bungo, akizungumza katika kongamano hilo aliwataka Waislamu na Wakristo kuungana kutafuta adui anayewachonganisha.

Aliitaka serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi kuwapa majibu ya kile kilichobainika na  Shirika la Upelelezi la Marekani FBI katika mauaji ya Padre Evaristus Mushi yaliyofanyika huko Zanzibar.

Sheikh Ponda ameyazungumza hayo siku chache tu baada ya kuhukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja kwa tuhuma za kuingia kwenye eneo la watu kinyume cha sheria.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment