Monday 3 June 2013

Ujio mwili wa Mangwea utata



KUWASILI kwa mwili wa aliyekuwa msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya nchini, marehemu Albert Mangwea ‘Ngwair’, aliyefariki Mei 28, mwaka huu, nchini Afrika Kusini, kumezidi kuwa tata.
Awali mwili huo ulitarajiwa kuwasili nchini juzi lakini ukaahirishwa huku ikielezwa ungefika jana mchana, napo ikashindikana, hivyo kuzua sintofahamu, kutokana na mipangilio ya kuusafirisha kutokwenda vizuri kama ilivyopangwa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, kaka wa marehemu, Kenneth Mangwea, alisema baada ya vikao vya familia jana jioni, wamepokea taarifa za kuwasili kwa mwili huo kama mambo yakienda sawa kesho.
Alisema awali iliripotiwa kuwa mwili huo ungeletwa kati ya juzi au jana ili kufanikisha taratibu zote za mazishi, lakini bado ukweli haujafahamika kutokana na ugumu wa mchakato wa usafirishaji.
“Taarifa tulizonazo ndizo hizo tulizozipokea hadi sasa, kwani tunawasiliana na ubalozi nchini Afrika Kusini ili kufahamu lini utawasili mwili wa marehemu, lakini kama tutapata taarifa mapema kupitia ubalozi tutawajulisha kitakachoendelea,” alisema Kenneth.
Kenneth alibainisha kuwa bado wanaendelea na taratibu za maandalizi ya mazishi hayo, kwa kukusanya michango nyumbani kwa baba yao mdogo, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambako wametenga msiba huo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment