Wednesday, 12 June 2013

Watanzania hatarini kupata mabusha, matende

IMEELEZWA kwamba Watanzania wote wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya mabusha na matende.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Dk. Edward Kirumbi wakati wa semina kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu uelewa wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Katika semina hiyo pia wataalamu wa magonjwa hayo walisema wakazi wa majiji ya Mwanza na Dar es Salaam watapewa dawa za magonjwa hayo kwa siku tano mfululizo kuanzia Juni 22, mwaka huu.
Aliyataja baadhi ya magonjwa sugu yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kuwa ni mabusha na matende, minyoo, kichocho, usubi, trakoma na kichaa cha mbwa ambayo husababisha ulemavu wa kudumu.
Dk. Kirumbi alisema maradhi hayo huenezwa na mbu aina ya Anopheles na Curex ambao hubeba vimelea vya minyoo hivyo kuwaweka Watanzania wote kwenye hatari hiyo bila kujali umri.

“Mbu anayekuambukiza malaria anaweza kukuambukiza mabusha au matende kwa sababu yanaambukizwa kwa minyoo midogo midogo iliyopo kwenye mfumo wa majimaji na damu,” alisema na kuongeza watu zaidi ya bilioni moja wapo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa hayo.
Awali, Dk. Upendo Mwingira, alisema Watanzania milioni 2.5 wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya trakoma huku akisisitiza kwamba magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yapo zaidi kwenye jamii maskini.
“Kwa vile yapo kwenye jamii maskini zaidi kwenye ukanda wa tropiki, mgonjwa hana sauti, yanaathiri ukuaji wa mtoto kiakili, yanazorotesha shughuli za maendeleo na kuzidisha umaskini,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Upendo ambaye pia ni Mratibu wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza magonjwa hayo (NTDCP) wamezifikia halmashauri 97 ambazo huzipatia dawa kila mwaka.
“Tunao mpango wa kwenda kwenye halmashauri nyingine kwa kuongeza majiji ya Dar es Salaam na Mwanza kwenye mpango wetu wa kugawa dawa mara moja kila mwaka hivyo tunaamini tutazifikia halmashauri zaidi ya 105,” alisisitiza.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment