Wednesday 31 July 2013

Hakimu acharuka kesi ya Kibanda

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliucharukia upande wa mashtaka katika kesi ya kuandika makala ya uchochezi inayomkabili aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na wenzake.
Hatua hiyo ni baada ya upande huo jana kushindwa kutoa mustakabali wa kesi hiyo kama walivyoahidi.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Waliarwande Lema, baada ya kumaliza kumsikiliza Wakili wa Serikali, Beata Kitalu, ambaye alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, alisema upande wa Jamhuri jana ulikuwa umepanga kutoa mustakabali wa kesi hiyo.
“Sasa leo unasema kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa. Kutajwa tu, kutajwa tu?” alihoji na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Kibanda washitakiwa wengine ni mwandishi wa waraka huo uliochapishwa Novemba 30, 2011, Samson Mwigamba na aliyekuwa Kaimu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Theophil Makunga.
Hadi sasa ni mashahidi watatu ambao wametoa ushahidi wao kwa upande wa Jamhuri tangu kesi hiyo ilipofunguliwa Desemba mwaka 2011.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment