Wednesday, 31 July 2013

Siku nne barabarani na uchungu wa uzazi

Nilitembea kwa miguu siku nne kwenda Ludewa kutafuta hospitali huku nikiwa na uchungu wa uzazi."
 
Aliyepata adhani hiyo ni Maria Haule, mkazi wa Lupingu, anayeishi kwa kutegemea kilimo kweye mwambao wa Ziwa Nyasa, mkoani Njombe.
 
Maria ana umri wa miaka 47, alilazimika kutembea kwa miguu kwenda hospitalini Ludewa baada ya kujifungua kienyeji nyumbani kwake Lupingu, lakini mfuko wa uzazi – Placenter ulichelewa kutoka.
 
Ukosefu wa huduma ya uzazi katika kituo cha afya cha Lupingu, ulisababisha Maria  kutembea kwa miguu hospitali ya wilaya ya Ludewa huku mfuko wa uzazi ukining’inia.

Mbali na zahanati ya Lupingu kukosa huduma ya uzazi, pia haina wataalamu, lakini pia umbali kati ya Lupingu na Ludewa ni tatizo ingine kwa sababu hakuna usafiri wa uhakika.


“Ilikuwa safari ngumu ya siku tatu, kupita mbugani usiku na mchana kabla ya kufika Ludewa siku ya nne, mfuko wa uzazi ukiwa unaning'inia,” anasimulia Maria.

Maria hajui umbali kati ya maeneo hayo, lakini anasema inachukua saa nane hadi 10 kutembea kwa miguu kutoka Lupingu kufika Ludewa.

Anasema yeye akiwa mgonjwa alishindwa kutumia muda huo kufika Ludewa, badala yake alifika siku ya nne baada ya safari ya siku tatu mbugani.

Kwa mujibu wa Maria, hospitali ya Ludewa inahudumia watu wengi ambao ni wakazi wa vijiji 76 vya wilaya hiyo.

Anasema juhudi ya kuomba msaada ili aweze kupata usafiri wa gari ilikwama kwa sababu kila aliyemfuatwa kuelezwa shida hiyo alikubali kusaidia lakini kwa malipo makubwa.
 
Anasema kutokana na hali hiyo ilibidi atembee kwa miguu baada ya kukosa fedha za kuwalipa wenye gari ili wamkibize kwenda hospitalini.

“Kabla ya kuamua kutembea niliomba watu wanisaidie, mmoja mwenye gari akaniambia nimlipe sh. 100,000, sikuwa na fedha kabisa,” anasema Maria.

Anasema baada ya kukosa msaada akaanza safari ya kuvuka vilima na mabonde, akilala njiani kila jua linapokuchwa.

Lakini anashukuru, baada ya kuwasili hospitalini madaktari wa hospitali ya Ludewa na wasaidizi wao walimhudumia haraka.

“Madaktari, manesi na wahudumu walisaidia sana kuokoa maisha yangu, hatimaye mfuko wa uzazi ulitoka,” anasema Maria.

Anaongeza kuwa, “kwangu ulikuwa muujiza madaktari waliponiambia wamefanikiwa kuutoa mfuko wa uzazi.”

Mtoto wa kiume wa Maria aliyezaliwa na kufuatiwa na tatizo la mfuko wa uzazi wa mama yake kugoma kutoka hivi sasa anasoma ana umri wa miaka mine.
 
Theresia Kiowi,  pia mkulima  wa Lupingu anasema ukosefu wa huduma ya uzazi ni tatizo sugu linalotishia maisha ya wajawazito.

Anasema mbali na Lupingu, vijiji vya Makonde, Lifuma, Sumba na Nsisi pia vina matatizo ya aina hiyo na pia ubovu wa barabara.
 
Ukosefu wa huduma ya uzazi hauathiri wazazi peke yao, kwani hata watoto wanaozaliwa pia wanakosa huduma mbali mbali za awali ambazo ni pamoja na chanjo.

Maria anajua hilo ni tatizo la maeneo mengi ya vijijini, lakini anaamini hali n mbaya zaidi Lupingu kwa sababu zahanati iliyopo inahudumia watu wengi.

Anasema pamoja na athari nyingine, ukosefu wa huduma ya uzazi kijijini ni hatari kwa sababu unaweza kusababisha wazazi kupoteza maisha wakati wa kujifungua.

Wataalam wanasema mama kujifungua kuna hatua nyingi, ni pamoja na mtoto kutoka salama na mfuko wa uzazi kutoka, usipotoka kwa wakati mzazi anaweza kupoteza maisha.

Apaa Nkya, ni ofisa muunguzi katika hospitali ya Lugalo, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) jijini Dar es Salaam.

Anasema kwa kawaida mfuko wa uzazi unapaswa utoke dakika chache, mara tu baada ya mama kijifungua salama.

Anasema hali ya mfuko wa uzazi kugoma kutoka inaweza kusababisha mzazi kupoteza maisha kwa kutokwa damu nyingi na vle vile iwapo atakosa huduma.

Apaa anasema chanzo cha mfuko huo kugoma kutoka kunasababishwa na matatizo mbali mbali ya kiafya, kama vile upungufu wa baadhi ya madini mwilini.

Anasema matatizo hayo yanatokana na mfuko huo kutojiachanisha kwa urahisi kutoka kwenye kuta za mji wa uzazi – Uterus.

Anasema mama anapokuwa mjauzito, mfuko wake wa uzazi ujitengeneza ndani ya mji wa uzazi, kama ilivyo kwa matunda ndani ya ganda lake.

Mfuko wa uzazi ukikosa aina fulani ya madini yenye kufanya usishikane, unang’ang’ania kwenye kuta za mji huo wa uzazi unaoitwa uterus, anasema Apaa.

Anasema njia inayotumika kuokoa maisha ya mama mwenye tatizo hilo, wataalamu huingiza mkono kupitia njia ya uzazi na kuutoa mfuko huo.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman  Kinana ni miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu nchini wenye uelewa wa kutosha juu ya matatizo ya uchumi na kijamii wilayani Ludewa.

Hivi karibuni alifanya ziara ya mkoa wa Njombe na miongoni mwa mambo aliyoshuhudia ni pamoa na huduma duni katika sekta mbali mbali, afya na barabara zikiwamo, ndio maana wakati wa ziara yake akaahidi zahanati hiyo itatengenezwa na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. 
 
Kinana pia aliahidi kupeleka Ludewa jumla ya mabati 500 na mifuko ya saruji 700 kwa ajli ya utengenezaji wa hospitali Lupingu.

Pamoja na Kinana Mbunge wa jimbo hilo Deo Filikunjombe kwa upande wake tayari ametoa sh. milioni 400 kwa ajili ya maboresho ya barabara kati ya Lupingu na Ludewa.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment