Akizungumza na NIPASHE muda mfupi baada ya tukio hilo, mke wa Sheikh Ponda, Khadija Ahmad, alisema saa 4:00 asubuhi, aliingia daktari ambaye hajawahi kumuona kwa kuwa siye aliyekuwa akimtibu mumewe.
Alisema daktari huyo alimwangalia mumewe kwa muda mfupi kisha akawaeleza kuwa mgonjwa anaendelea vizuri, hivyo ameamua kumruhusu.
Kwa mujibu wa Khadija, walipinga jambo hilo kwa kuwa hali ya mumewe waliona kuwa ilikuwa bado haijatengamaa.
Hata hivyo, alisema daktari huyo alishikilia msimamo wake na kutoka nje ya chumba alicholazwa Sheikh Ponda.
Alisema baada ya muda mfupi, waliingia askari kanzu wengi na kumchukua Sheikh Ponda bila kusema wanakompeleka.
Khadija alisema kitendo hicho kiliwafanya wahoji na kwamba mmoja wa askari akajibu kuwa wao siyo wasemaji.
Alisema askari mwingine aliwataka kutokuwa na wasiwasi kwani Sheikh Ponda yupo kwenye mikono salama na kwamba anapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi na baada ya hapo atapelekwa katika mahabusu ya Segerea.
“Wamemlazimisha daktari kumtoa mume wangu wakati hali yake bado haijatengamaa. Haina maana kabisa kumweka ndani mtu mwenye hali kama ile. Bado anaendelea na matibabu,” alisema Khadija.
NIPASHE ilishuhudia Sheikh Ponda akitembea kwa kusaidiwa na askari hao na hakufungwa pingu.
Askari hao walimpitisha kwenye mlango wa dharura na kumuingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser Hard Top la kampuni ya Antelope Safaris lenye namba za usajili T 140 BLA na kuondoka hospitalini hapo, huku likifuatwa na magari mengine matano ya polisi, Defender tatu pamoja na Toyota Land Cruiser mbili.
Akizungumzia tukio hilo, Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro, alisema kilichofanyika kwa mteja wake hakiko sawa kwa kuwa Sheikh huyo alishasomewa mashtaka na yupo chini ya mahakama kwa hiyo walitakiwa kupata kibali cha mahakama kitu ambacho hakikufanyika.
“Na hoja nyingine ni kwamba, jana alikuwa afanyiwe mahojiano, lakini hayakufanyika kwa sababu za kiafya na alikuwa anasikia maumivu kwenye jeraha pamoja na kichwa. Na leo (jana), kumtoa hospitali na kumpeleka magereza ni kitendo cha kumuumiza zaidi,” alisema Nassoro.
Alisema kwa sasa wanafikiria cha kufanya na watatoa taarifa hivi karibuni.
Naye msemaji wa familia ya Sheikh Ponda, Ishaka Rashid, alisema suala la Sheikh huyo, wanalirudisha kwenye taasisi za Kiislamu pamoja na wafuasi wake, kwani awali walikuwa wameziomba zisichukue taratibu zozote ambazo zingeathiri hali ya matibabu yake.
“Sisi kama wanafamilia tumeamua kurudisha suala hili kwa taasisi.
Hivyo wao ndiyo wataamua ni namna gani watalishughulikia kuhakikisha usalama wake,” alisema Rashid na kuongeza:
“Polisi wamemteka mgonjwa. Tumekubaliana kuwa mambo mengine yatafuata baadaye.
Kwani kwa sasa tunayapa matibabu ya mgonjwa umuhimu wake. Hawajafanya jambo jema. Na cha kushangaza wameacha hata dawa zake,” alisema Rashid.
Alisema mazingira ya kuchukuliwa kwake yanatia shaka kwa kuwa familia haikujulishwa ni wapi alikopelekwa.
Kwa mujibu wa Rashid, hofu ya Sheikh Ponda kudhuriwa bado iko pale pale kwa kuwa polisi ndiyo waliompiga risasi.
Kwa upande wake, Meneja wa Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alisema Sheikh Ponda aliruhusiwa kama taratibu zinavyotaka.
“Huyo mgonjwa amesharuhusiwa na kwa sasa hayupo hapa,” alisema Almasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alipotakiwa na NIPASHE kueleza suala hilo, alimtaka mwandishi amuulize Kamanda wa Kanda Maalum, Suleiman Kova.
“Mimi sihusiki na wala siyo msemaji mkuu wa suala hilo. Hivyo, inatakiwa aulizwe Kamanda Kova, kwani yeye ndiye msemaji wa hilo,” alisema.
Kamanda Kova alipoulizwa, alikataa kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba suala la Sheikh Ponda liko mahakamani, hivyo taarifa zote zipo Mahakama ya Kisutu.
“Kwa sasa sisi kama Jeshi la Polisi hatuna mamlaka ya kuzungumzia jambo hili kwa kuwa tayari lipo mahakamani na kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa mahakama,” alisema Kova.
Wakati huo huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi (SSP), Advera Senso, akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana alisema jeshi hilo linamshikilia afisa wao mmoja aliyefyatua risasi hewani kwenye safari ya Sheikh Ponda, mkoani Morogoro, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kumekuwapo na kauli zinazokinzana kati ya Jeshi la Polisi na Sheikh Ponda, ambaye yeye na wafuasi wake wakidai kuwa alipigwa risasi, lakini jeshi hilo likikanusha madai hayo.
Hata Moi ambako alilazwa, walisema kuwa walikuwa hawakugundua kwa kuwa hawakumfanyia upasuaji na kwamba taarifa hizo walipaswa kuwa nazo Hospitali ya Islamic Foundation ya mkoani Morogoro, ambao ndiyo waliomfanyia upasuaji.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment