Tanga. Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, jana ilianza hatua ya awali ya kusikiliza mashtaka ya mauaji yaliyozua gumzo mkoani Tanga yanayomkabili Philemon Mwakamale anayedaiwa kumuua kwa kumkata na jembe Wema Gigo.
Mashtaka hayo yanasikilizwa na Jaji wa Mahakama hiyo,Pendo Msuya,ikisimamiwa na mawakili wa Serikali Mwasiti Athumani na Shose Naiman huku kwa upande wa utetezi anawakilishwa na Obadiodom Chanjarika.
Ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Mwasiti Athumani mbele ya Jaji Msuya kuwa, April 26 mwaka 2010 katika shamba la marehemu Wema Gigo lililopo Kijiji cha Mbogo, Wilaya ya Kilindi Mkoa wa Tanga, mshtakiwa alimuua Gigo kwa kumkata kichwani na jembe.
Aliendelea kudai kuwa mshtakiwa alikwenda shambani kwa Wema Gigo akamkuta akilima ndipo akamnyang’anya jembe na kutenda kosa hilo kisha akachukua mwili wa marehemu na kuufukia chini na kufunika majani.
Wakili huyo wa Serikali alidai, wakati mshtakiwa akitenda tendo hilo,jirani alikuwapo Rawlent Kiliani aliyekuwa akimuona na alipobaini kuwa kuna mtu pembeni akaanza kumfukuza huku akimsihi asimtaje.
Hata hivyo, Rawlent alipiga mayowe ndipo watu wakakusanyika na kumkuta Wema akiwa amefukiwa na majani ndipo wakamchuku na kumpeleka ofisi ya kijiji cha Mbogo ambako baada ya muda mfupi alikufa.
Baada ya kusomwa mashtaka hayo Wakili wa utetezi, Chanjarika alisimama na kukubali kwamba mshtakiwa alikamatwa na ameshtakiwa lakini alikana mashtaka yote yaliyosomwa dhidi ya mteja wake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi mahakama kuu kanda ya Tanga itakapopanga tarehe nyingine kwa lengo la kuanza kusikiliza mashahidi ambao upande wa mashtaka wapo tisa huku mshtakiwa akiwa na shahidi mmoja.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment