Saturday, 5 October 2013

Maiti ya mtoto wa miezi 10 yachunwa ngozi

MAMIA ya wananchi mjini Bunda, wamefurika kushuhudia mwili wa mtoto wa miezi 10 aliyefariki kwa ugonjwa wa malaria na baadaye watu wasiofahamika kuchuna ngozi ya kichwa chake.
Tukio hilo ambalo limehusishwa na imani za ushirikiana, lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika mtaa wa Nyasura ‘B’ Tarafa ya Serengeti katika mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, wilayani hapa.
Ofisa tarafa, Justine Rukaka, alisema kuwa mtoto huyo alifariki usiku katika hospitali ya wilaya ya Bunda, baada ya kuugua malaria na mwili wake ukapelekwa nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi.
Rukaka alisema kuwa kesho yake asubuhi wakati wananchi wanaandaa shughuli za mazishi, walishangaa kuona ngozi ya kichwa chake ikiwa imechunwa na watu wasiofahamika.
“Wakati shughuli za mazishi zinaandaliwa ndipo walipogundua kuwa ngozi ya kichwa chake imechunwa kwa kile kinachodaiwa kwamba ni imani za ushirikina,” alisema.
Aliongeza kuwa kufuatia hali hiyo, wazazi wa mtoto huyo, wanafamilia pamoja na waombolezaji wengine walijawa na hofu kubwa kwamba tukio hilo lilikuwa la kishirikina.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, shughuli za mazishi zilikwama kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi jioni, ambapo polisi wakiwa na daktari walifika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huku wananchi wakitulizwa wasifanye vurugu.
Ofisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Mara, Jafari Mohamed, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.   Hili ni tukio la pili kutokea mjini hapa, ambapo hivi karibuni mtoto wa umri kama huo pia alifariki kwa ugonjwa wa malaria na kesho yake wakati shughuli za mazishi zinaandaliwa alikutwa amekatwa mdomo.

No comments:

Post a Comment