Saturday, 2 November 2013

MWANAMKE aliyepigwa risasi ya bega na askari polisi azua jambo!

MWANAMKE aliyepigwa risasi ya bega na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) jijini Arusha juzi, Vaileth Mathias, ameibua gumzo baada ya kuzuiliwa asionwe na watu mbalimbali wakiwamo waandishi wa habari.
Vaileth alijeruhiwa kwa risasi baada ya kudaiwa kumtishia kwa bastola polisi aliyekuwa kwenye lindo katika Benki ya CRDB, ambapo mwanamke huyo alizuiwa kuegesha gari lake.
Hatua hiyo ya kufichwa kwa mwanamke huyo iliibua taarifa za hapa na pale kwa wananchi huku wengine wakimhusisha kuwa na mahusiano ya karibu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Kwa sasa Vaileth anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre(ALMC), maarufu kwa jina la Selian.
Juhudi za waandishi wa habari waliofika hospitalini hapo jana saa tatu asubuhi kwa ajili ya kumuona, ziligonga mwamba baada ya mtumishi wa mapokezi ya hospitali hiyo kuwataka wasubiri ili apate maelekezo kutoka kwa viongozi wake.
Wakati waandishi wakiendelea kusubiri, aliingia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, kwa ajili ya matibabu na alipohitaji kumuona mgonjwa huyo alizuiwa hadi alipotoa kitambulisho ndipo aliruhusiwa kuingia kumuona huku wale aliokuwa wameambatana nao wakizuiwa nje.
Baada ya nusu saa, mhudumu wa mapokezi aliwaeleza waandishi kuwa katibu muhtasi wa ofisa tawala wa hospitali hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alimweleza kwamba mgonjwa amesema hahitaji kukutana na vyombo vya habari.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, ili kutoa taarifa zaidi juu ya tukio hilo kama alivyoahidi juzi, alidai kuwa anaumwa, hivyo anakwenda hospitali.
Alipobanwa aeleze kama silaha aliyokuwa nayo Vaileth anaimiliki kihalali na wanatarajia kumfungulia mashitaka gani ikibainika alimtishia askari, Sabas aliendelea kutembea kuelekea kwenye gari lake huku akidai upelelezi haujakamilika.
Pia alikanusha kuwa jeshi hilo halihusiki kwa namna yoyote na ulinzi uliopo kwenye chumba cha mgonjwa huyo.
“Ninaenda hospitali, sukari yangu haiko vizuri, uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea, hivyo hayo masuala ya bastola siwezi kuyaongelea kwa sasa, taarifa bado iko vilevile kama nilivyoeleza jana,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alipopigiwa simu kuulizwa kama ni kweli ana mahusiano ya karibu na Vaileth, kwamba ndiyo sababu alikuwa na jeuri ya kuwatisha polisi kwa silaha, hakukubali wala kukanusha, badala yake alihoji: “Tatizo liko wapi?
“Ni vema kuzungumzia tukio lenyewe, wasiliana na kamanda wa polisi kwani ndiye mwenye taarifa sahihi,” alisema kisha alikata simu.
Juzi baada ya Vaileth kufikishwa hospitalini hapo wapiga picha na waandishi walipata wakati mgumu kumfikia kutokana na kiongozi mmoja wa wilaya kuwazuia hadi kufikia katua ya kukingakamera ili wasiweze kupata picha.
Vaileth alidaiwa kukaidi amri ya polisi ya kumtaka asiegeshe gari lake kwenye eneo la lango la kuingilia Benki ya CRDB Tawi la Mapato na ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Arusha, hivyo polisi waliamua kulitoa upepo.
Baada ya kutoka ndani na kukuta gari lake limetolewa upepo kwenye magurudumu, alikasirika na kutoa bastola huku akiwafuata askari, ndipo katika kujihami mmoja wao alimpiga risasi ya bega la kushoto.
Katika hatua nyingine, inadaiwa kuwa Vaileth ni mmoja wa wahitimu wa stashahada ya masoko, aliyeanza masomo Agosti 2011 katika Chuo Kikuu cha Mount Meru, ambapo mahafali yao yanatarajiwa kufanyika kesho.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment