JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kumvamia, kumjeruhi kwa mapanga na kupora mali za Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi (61).
Dk. Mvungi ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kisheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi bado amelazwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu (ICU) cha Taasisi ya Mifupa (Moi) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili huku hali yake ikidaiwa kuimarika taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la Moi, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema licha ya kutopata fahamu tangu afikishwe hospitalini hapo, afya yake inaendelea vema.
“Tangu alivyofikishwa hapa juzi alfajiri, hali yake ilikuwa mbaya sana… haina maana kwamba sasa hivi ni nzuri ila ina afadhali kuliko awali.
“Hajapata fahamu ya kumtambua mtu ndiyo maana jopo la madaktari kila wakati wanapishana kuingia kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu kwa ajili ya kuhakikisha afya yake inaimarika,” alisema Mbatia.
Dk. Mvungi, aliyewahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipatwa na mkasa huo usiku wa kuamkia Novemba 3, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Watu hao wanaokariwa kuwa sita, walivamia nyumba ya Dk. Mvungi ambaye pia Mhadhiri wa Chuo cha Bagamoyo (UB) na kumjeruhi kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Baada ya kumjeruhi waliiba sh milioni moja, bastola, simu mbili za mkononi na kompyuta mpakato (laptop) mali za gwiji huyo wa sheria nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna wa Kanda hiyo, SuleimanKova, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kubainisha kwamba muda mfupi baadaye askari polisi walianzisha operasheni kuanzia maeneo ya Mpigi Majohe kwa kushirikiana na raia wema.
“Tulianzisha msako mkali eneo hilo… hatimaye kuna watu tuliwatilia mashaka, hivyo tukaamua kuwakamata kwa mahojiano zaidi,” alisema Kkamishna Kova na kuongeza kwamba watuhumiwa hao walipekuliwa, wakakutwa na bangi puli 17 na gongo lita 15.
Kwa mujibu wa Kova, kuna msako mkali unaowahusisha askari wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam ili kuhakikisha wahusika wanapatikana na kufikishwa mahakamani.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, juzi jioni walifika Moi ili kumjulia hali Dk. Mvungi.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment