Monday, 13 January 2014

Mbowe kumburuza Zitto mahakamani

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), anakusudia kumburuza mahakamani, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa madai ya kumkashifu na kumchafulia jina.
Kwa mujibu wa taarifa toka Kurugenzi ya  Habari na Uenezi ya CHADEMA, Mbowe amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza.
Tayari Mbowe kwa mujibu wa taarifa hiyo, ameshawasiliana na wanasheria wake kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya aliyezusha uongo huo.
Ingawa taarifa hiyo haikutaja jina la Zitto, lakini hivi karibuni mbunge huyo katika ukurasa wake wa facebook, aliibua tuhuma nzito dhidi ya Mbowe.
Zitto, Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo, walivuliwa nyadhifa zao na Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA.
Baadaye CC iliwatimua uanachama Mwigamba na Kitila kwa tuhuma za kukisaliti na kukihujumu chama, huku Zitto akikimbilia mahakamani kuzuia asijadiliwe.
Akiwa na kesi mahakamani, Zitto aliingia mtegoni kwa kushambulia viongozi wake mitandaoni kwa kutoa tuhuma nzito dhidi ya Mbowe.
Katika tuhuma hizo, Zitto alidai Mbowe alipokea michango ya pesa kutoka kwa makada wa CCM, Nimrod Mkono na Rostam Azizi, kusaidia kampeni za CHADEMA mwaka 2005 na 2010.
Pia Zitto alidai kuwa Mbowe alipokea sh milioni 40 mwaka 2005 kutoka kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini; na kwamba mwaka 2008 alimpatia sh milioni 20 kusaidia CHADEMA ishinde uchaguzi mdogo wa Tarime.
Kutokana na tuhuma hizo, CHADEMA kupitia ofisa wake wa habari mwandamizi, Tumaini Makene, jana iliamua kujibu mapigo.
Katika taarifa yake, ilisema tuhuma hizo ni moja ya mikakati ya Zitto na wenzake wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama.
“Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe, amezushiwa tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake.
“Tuhuma hizo ni pamoja na kwamba, Mbowe mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka kwa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kiasi cha sh milioni 40 ili Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.
“Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono alimpatia Mbowe sh milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye chama kama mkopo na akalipwa.
“Mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mbunge Mkono eti alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa Mbowe sh milioni 200 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.
“Mwaka huo huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa, alipokea sh milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
“Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kusema yafuatayo: Hakuna ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. Ni uongo na uzushi uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM, na kwamba chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania katika kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi, kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho kimepoteza ushawishi kwa wananchi.
“Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
“Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko nchini kwamba, Mbowe  ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.”
Taarifa hiyo iliwataka Watanzania wote, hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko wote nchini, kwamba; CHADEMA wala Mbowe mahali popote na wakati wowote, hawajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.
“Tungependa kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda kutunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA, badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya msingi yanayowaandamana kuhusu mikakati yao ya kuhujumu CHADEMA na viongozi wake,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema iwapo chama kisingeibaini mikakati hiyo na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.
Makene alisema katika taarifa hiyo kwamba kuhusu baadhi ya tuhuma katika mkakati huo ambazo zimemlenga Mbowe kwa kuhusisha shughuli zake binafsi za uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi husika.
Hata hivyo, tayari Mbunge Mkono alishatoa ufafanuzi kupitia gazeti hili kwamba hajawahi kumpa Mbowe hata senti tano, na kwamba hizi ni siasa za majitaka.
Rostam Aziz naye akijibu tuhuma hizo zilizotolewa na Zitto alisema: “Miaka miwili iliyopita nilitangaza kujitoa katika siasa za ushindani ambazo kwa mtazamo wangu zilishafikia kiwango cha kuitwa siasa uchwara. Sioni kama itakuwa busara kwangu kuniingiza katika malumbano mapya tena.
“Siku zote nimekuwa kimya kila jina langu linapotajwa kwa namna na kwa njia tofauti katika vyombo vya habari. Naona ni busara kwangu nikiendeleza hekima hiyo ya kukaa kimya na kuacha ukweli ukinitetea.”
Mbowe mwenyewe alisema hajawahi kupokea pesa hizo
chanzo:tz daima

No comments:

Post a Comment