WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutoruhusu mtu yeyote kununua urais kama njugu.
Alitahadharisha kuwa kama itatokea kada yeyote wa CCM amepata urais kwa kununua kama njugu, waandishi wa habari nchini watakuwa wa kwanza kulaumiwa kwa kuwasaidia kuwaingiza madarakani watu wa aina hiyo.
Ingawa Waziri Membe hakutaja jina la mtu, lakini kauli yake ni dhahiri kwamba ilikuwa ikimlenga Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye amekuwa akiandamwa ndani ya chama chake, kwamba anataka urais kwa kumwaga fedha katika vikundi mbalimbali nchini, kikiwemo chama cha waendesha Bodaboda.
Waziri Membe alitoa kauli hiyo ya fitna jana mjini Dodoma mara baada ya kumaliza kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, chini ya uenyekiti wa Philip Mangula.
Membe ambaye ni miongoni mwa watu wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015, aliitaka CCM iwe makini kufuatilia nyendo za makada wake wanaotaka urais kwa kumwaga fedha ili wachukuliwe hatua.
“CCM hakiwezi kuruhusu urais wa nchi upatikane kwa kununua kama njugu na kama itatokea hivyo waandishi wa habari mtakuwa sehemu ya lawama.
“Waandishi nawambia mtaona tukiacha suala hilo litokee hapa nchini kwani hamuwezi kututengenezea uongozi kwa njia ya fedha,” alisema Waziri Membe.
Alisisitiza kuwa ni mwiko kwa mtu yeyote ndani ya CCM kutumia fedha kama nguzo ya ushindi kama wanavyofanya baadhi ya makada ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina.
Akizungumzia mambo yaliyojitokeza kwenye mahojiano yake na Kamati ya Maadili, Waziri Membe alieleza mambo makubwa matatu na kubwa kuliko yote ni kuibuka kwa makundi ya urais.
Suala la pili alisema ni matumizi ya fedha katika kuusaka urais kwani alidai kuwa kuna watu wanatumia mabilioni ya fedha kujiimarisha kisiasa kwa ajili ya urais mwakani.
“Suala la tatu ni ninyi waandishi wa habari. Sijui mmelishwa nini? Sijui mmemeza mdudu gani vichwani mwenu mpaka muone kinachosemwa na mtu fulani ni cha maana kitoke kwenye magazeti na kingine kikisemwa na fulani hata kama ni cha maana kisitoke kwenye magazeti,” alisema.
Membe alisema katika majadilino na kamati hiyo, walijadili uwezekano wa kuwapata wagombea urais ifikapo Desemba mwaka huu ili kumaliza fitna na makundi yanayoweza kukimega chama.
“Hayo yalikuwa sehemu ya majibu yangu na niliitaka kamati hiyo iendelea kufanya kazi hiyo na bado kuna watu wengine waitwe lengo likiwa kukifanya chama kiwe imara na kiende kwenye uchaguzi mwakani kuvishinda vyama vyote vinavyojitokeza tokeza na vingine ambavyo vimeanza kufa,” alisema Waziri Membe.
Kwa mujibu wa Membe, aliishauri kamati hiyo kuhakikisha chama kinaandaa midahalo kwa ajili ya makada wake wanaowania urais ili wananchi wawajue mapema na hata uwezo wao wa kujieleza.
Waziri Membe alijigamba kuwa CCM ndiyo inaweza kuamua muelekeo na hatma ya nchi na wasipokuwa makini kwa kuwaacha wenye pesa kuchukua uongozi, chama kitakufa na taifa litaangamia.
Kamati Ndogo ya Maadili yenye wajumbe sita, ilianza kuwahoji makada wake wanaodaiwa kukiuka kanuni za chama hicho Februari 13.
Mbali ya Membe ambaye jana alifunga dimba, wengine waliowekwa kitimoto na kamati hiyo ni pamoja na Lowasa, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Sayansi na Tecknolojia, Januari Makamba.
chanzo:tz daima
No comments:
Post a Comment