SIKU moja baada ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC) kukata matangazo ya moja kwa moja wakati Bunge la Katiba likiendelea mjini Dodoma, wanasiasa na wananchi wa kada mbalimbali wamelaani na kutaka kituo hicho kiwaombe radhi Watanzania.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema TBC ni adui namba moja wa wananchi.
Dk. Slaa alisema kitendo cha TBC kukata matangazo waka
ti Tundu Lissu akizungumza hakukishangaa kwani ni kawaida ya kituo hicho kuhujumu demokrasia.
Alisema TBC imejisahau kuwa ni chombo cha wananchi ambao wanakatwa kodi kwa ajili ya kukiendesha kituo hicho, lakini wamekuwa wakikitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Slaa alisisitiza kuwa TBC ni adui namba moja wa Watanzania wapenda mageuzi na mpotoshaji wa mambo yanayowahusu wananchi.
“Wabunge wakizungumza kinyume na matakwa ya CCM wanakata matangazo, hizo ni propaganda zinazoendeshwa na chama hicho, wamesahau kuwa Watanzania wanalipa kodi,” alisema.
Alisema serikali imesahau kwamba ilisaini maadili ya vyombo vya umma ili vitumike kwa manufaa ya umma.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Watanzania wanapaswa kutambua kuwa adui mkubwa si CCM aliyodai imewapa maisha magumu,bali pia adui mwingine ni TBC na propaganda zake.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana, alisema kukata matangazo kwa kuficha maoni yenye mtazamo tofauti na wa CCM, hakuimarishi demokrasia ya kweli.
Alisema TBC wanapaswa kufahamu kuwa wanaendeshwa na fedha za walipa kodi.
Profesa Bana alisema uongozi wa TBC haupaswi kufanya vitendo hivyo kwani havitoi picha nzuri na haviungwi mkono.
“Wanapaswa waonyeshe kila kitu kinachoendelea bungeni kwani ni haki ya wananchi kusikiliza na kuangalia kile wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba anachosema,” alisema.
Mbali ya Dk. Slaa na Profesa Bana, mkazi wa Kimara, jijini Dar es Salaam, Andrew Donald, alisema kitendo cha TBC kukata matangazo na kuyarejesha wakati Lissu amemaliza kuzungumza si cha kiungwana.
“Wao wangeyaacha tu, kama kazungumza pumba sisi wananchi ndio tunajua, kama kazungumza yenye mantiki kwa taifa sisi wananchi tunajua, lakini kitendo cha kukata matangazo ni kukosa demokrasia na kuonyesha kuwa wanaendeshwa na CCM.
“Sikuelewa nini kilitokea ghafla hadi matangazo yakatizwe, kama walitumwa na mmoja wa viongozi wakubwa, wajue wanawanyima haki wananchi ambao wanapaswa kufuatilia kila kinachoendelea Dodoma,” alisema.
Donald alikumbushia tukio jingine la aina hiyo ambapo alisema TBC iliwahi kukata matangazo ya mkutano wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika Jangwani na hata kipindi maalumu cha mahojiano cha Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwa sababu wanazozijua kama walivyofanya kwa Lissu.
“TBC ilipokatiza kurusha moja kwa moja mkutano wa CHADEMA mwaka 2010 wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu kule Jangwani mvua ilinyesha, au walipokata matangazo ya Lowassa, kulikuwa na mvua?” alihoji.
Wakati wananchi wakiilalamikia TBC kukata matangazo ya moja kwa moja bungeni, uongozi wa kituo hicho ulitoa taarifa ya kujitetea.
Taarifa yaa TBC iliyotolewa juzi ilisema kuwa mvua iliathiri mitambo wakati wa hotuba ya Lissu.
“Kufuatia malalamiko ya watu wengi kuwa TBC ilikata matangazo kwa makusudi ili Lissu asiruke hewani, sio sahihi.
“Tunapenda Watanzania wajue kuwa huu ni msimu wa mvua na mitambo huathirika sana na maji. Hiyo ndiyo sababu na si vinginevyo. Ikumbukwe kuwa hakuna yeyote anayemuogopa Tundu Lissu.
“Si serikali wala si uongozi wa TBC, yeye ni mjumbe wa kawaida tu wa Bunge hili kama walivyo wajumbe wengine,” ilisema taarifa hiyo.
TBC ilikata matangazo yake mwishoni mwa wiki yaliyokuwa yakirushwa moja kwa moja wakati Lissu akiwasilisha maoni ya wajumbe wachache.
Ulipofika wakati ambao Lissu alianza kutoa takwimu, kufafanua na mifano mbalimbali ya watu waliouzungumzia upungufu wa Muungano na nini kifanyike ili kunusuru hali hiyo, ndipo matangazo hayo yalikatizwa ghafla, jambo ambalo lilisababisha Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kuahirisha Bunge na kuagiza Lissu aendelee kutoa maoni yake leo ‘live’.
chanzo:tz
No comments:
Post a Comment