Monday, 14 April 2014
Mtoto uliyemkana sasa anataka kukusaidia nawe hutaki, kwanini?
Naam. Simulizi iko hivi; Ipo familia moja iliyoishi ndani ya ndoa katika muda mfupi kisha mume akamfukuza mkewe. Kufukuzwa huku kulitokana na mizozo ya mara kwa mara na inavyoonekana, bwana yule alikuwa anazuzuliwa na mwanamke mwingine nje ya ndoa, ambaye baadaye ilithibitika pale alipomuoa mara tu alipomtimua yule wa kwanza.
Mama huyu aliyetimuliwa, kumbe alikuwa tayari mjamzito kwa mumewe. Hata hivyo, akahangaika huko na kule akabahatika kuanzisha mradi wa kuuza pombe haramu ya gongo ili mradi tu aweze kuishi na kumtunza mwanae wa kiume aliyemzaa.
Hata alipomtafuta mumewe huyo na kumjulisha kuhusu mtoto huyo alimkana kwamba siyo wa kwake kwa hiyo asijisumbue. Alipojaribu kujichanganya na watoto wenzake ambao baba yake alizaa na mama aliyeolewa baada ya mamake kutimuliwa, wenzake hao walimkana mtoto kwamba siyo wa familia yao.
Kijana huyu alikuwa vema mama akamsomesha kwa shida huku akihemea misaada kwa ndugu zake. Akabahatika kujiunga na jeshi ambako nako nyota yake iling’ara akawa katika nafasi nzuri iliyompandisha katika cheo kikubwa.
Kijana akamwanzishia mama yake miradi mbalimbali ya kiuchumi maisha yake yakabadilika kabisa. Lakini kila wakati akawa anamsisitizia mama yake ampeleke kwa baba yake. Ndipo mama alipoondoka naye hadi kwenye kijiji aliko babake huyo.
Kufika pale mama akawatafuta wazee wa kijiji kwanza na kujitambulisha kuhusu kilichowaleta.
Wakati huo kijana alifika akiwa na walinzi kutokana na cheo chake cha kijeshi. Ndipo mmoja wa wazee akajitolea kwenda na kijana kumuona baba yake. Kufika pale baba wa kijana kuwaona akataka kuondoka, ndipo yule mzee akamwambia usiondoke kwani ugeni huu ni wa kwako.
Mzee wa kijiji akawatambulisha mama na mwanae kwa yule baba kwa maelezo kuwa alipomfukuza mkewe kumbe alikuwa mjamzito na mtoto aliyezaliwa ndiye huyu aliyekuja kumuona. Yule baba akakana tena kabisa kumtambua kijana yule.
Katika hatua hiyo ikawa imeshindikana. Basi mzee wa kijiji, mama na mwanae wakaondoka ila wakapeana ahadi na wazee pale kijijini kwamba upo wakati watarejea tena.
Lakini kabla ya kuondoka, kijana akawauliza wazee wale kama baba yake huyo anayemkana analo shamba, wakamwonyesha na kisha wakaondoka zao. Kijana kurejea kazini kwake akajiandaa kumjengea baba yake japokuwa hakumtambua.
Alichofanya baada ya hapo ni kuandaa vifaa vya ujenzi na haraka akafika tena kijijini na kuamuru ujenzi ufanyike haraka hadi nyumba kukamilika. Ilipokamilika kijana akawaita tena wazee wa kijiji pamoja na baba yake ili amkabidhi.
Baba bado akaendelea kuikataa hata ile nyumba na ndipo kijana akanawa mikono kwani alidhani ni zawadi muhimu sana kwa baba yake. Akaondoka zake.
Katika hatua nyingine ikaelezwa kwamba baba huyu alihusishwa katika kesi ya mauaji pale kijijini kisha kufungwa. Yule baba akawa anatakiwa atoe sh. milioni mbili ili aweze kutolewa.
Katika mawazo yake akamkumbuka mkewe aliyemfukuza awali kwamba ndiye pekee angeweza kumnusuru kwa kuwa anazo fedha.
Akasuka mpango na askari ili amtoe gerezani humo kwa siri kisha wakamuone mkewe huyo wa kwanza kumuoma awasaidie hizo fedha.
Na walipomuendea mama kidogo akasita kutoa fedha zile kwa maelezo kuwa endapo mwanaye mwanajeshi atajua kuwa amemsaidia baba huyo aliyemkana, hatamsaidia tena.
Hata hivyo, kwa huruma aliyokuwa naye mama juu ya mumewe wa zamani, akazitoa fedha zile kwa masharti kuwa asitajwe kuwa ndiye aliyezitoa. Ndipo baba yule akafanikiwa kutolewa gerezani.
Baada ya kutolewa gerezani akawatafuta tena wale wazee akiwaomba wamuitie yule kijana amuombe msamaha na kumkubali kuwa ni mwanaye.
Wale wazee walipomwendea kijana na kumweleza dhamira ya baba yake aliyemkataa, naye akasema hawezi tena kwenda kumuona baada ya jitihada zote za awali kushindikana.
Mpenzi msomaji, hapo ndipo msimuliaji wa kisa hiki alipoishia kwa maelezo kuwa hajui nini kilichoeldelea baada ya hapo. Hii ni simulizi ya ukweli siyo ya kutunga.
Sasa tujiulize, kwanini mtu anamkana mwanaye hata pale sura inapolandana naye? Si unajua mtoto wa nyoka ni nyoka na hawezi kuwa mjusi? Na je, kitanda chaweza kuzaa haramu? Sasa kwanini baba anajua fika alikuwa na mahusiano na mama fulani, mtoto akazaliwa tena anayefanana naye kwa alama zote, lakini anamkana eti siyo wake? Laana gani hii?
Angalia baba huyu alivyokosa bahati iliyomjia mlangoni lakini akaipiga teke. Lakini baadaye pamoja na kupigwa teke ikamrejea tena imuinue lakini bado akaishindilia teke lingine la nguvu. Hivi watu hatujui kuwa tukisema ukweli utatuweka huru kama maandiko matakatifu yatuambiavyo?
Mama yule alisema ukweli kuwa mimba ile ni ya mumewe na hata mtoto alipozaliwa sura zikalandana kabisa, lakini bado baba akamkana. Na kibaya zaidi baba huyu akanyea kambi akijua kuwa hatairejea tena. Maisha hayako hivyo. Angalia mama aliyemfukuza pamoja na mtoto akiwa tumboni ndio waliokuja kumuokoa baadaye.
Huruma ya mama alimtoa gerezani kwa fedha ambazo mtoto aliyemkataa ndiye aliyezitoa. Na mtoto huyu huyu ndiye aliyemjengea nyumba nzuri kuliko zingine pale kijijini, japo pia aliikataa awali na sasa ndipo alipoegemeza ubavu wake.
Haya, si unajua majuto ni mjukuu? Baba huyu baada ya misukosuko, anafunguka na kutambua kosa lake, sasa anakiri kuwa kijana ni mwanae na anamuomba msamaha arejee kundini na kuwa sehemu ya familia.
chanzo:Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment