Thursday 24 April 2014

Haya ndio makavu laivuuu ya Dk. Mwinyi aliyowapa CCM.

Mjumbe  wa Bunge la Katiba, Dk. Hussein Mwinyi, ameeleza jinsi kero zilizopo ndani ya muundo wa Muungano wa serikali mbili zinavyoweza kutatuliwa na kuuponda muundo wa serikali tatu.
 
Akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, sura ya kwanza na ya sita bungeni jana, Dk. Mwinyi alisema Watanzania wanachotaka ni kuondolewa kwa kero za Muungano zilizopo, na si kutwishwa mzigo wa kugharamia serikali tatu.

 “Katiba ina mambo makuu mawili, kwanza ni lazima ihakikishe amani inakuwapo na pili inatakiwa kuleta ustawi wa jamii, kwa hiyo tunapojadili tunapaswa kuzingatia haya,” alisema.


Dk. Mwinyi, alianisha kero zinazolalamikiwa na kueleza jinsi ya kuzitatatua kikatiba ndani ya muundo wa sasa wa serikali mbili.

Alizitaja kero hizo kwa upande wa Zanzibar kuwa ni, ushuru wa forodha, uhuru wa kujiunga na taasisi za kimataifa, mambo ya muungano na mgawanyo wa ajira.

“Mambo haya hayahitaji serikali tatu kuyatatua, hii ni fursa sasa ya kuyatatua kikatiba ndani ya muundo wa serikali mbili.

Kwa mfano kero ya ushuru inaweza kutatuliwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ya Zanzibar kuondoa tofauti ya kodi ili iwe moja, kwa upande wa kero ya Zanzibar kuzuiwa kujiunga na taasisi za kimataifa iruhusiwe kwani kuna shida gani ya kujiunga OIC tena kwa sababu za kiuchumi,” alisema na kuongeza:
 
“Kero ya mgawanyo wa ajira uwekwe utaratibu utakaohakikisha kunakuwapo na uwiano mzuri wa ajira za Muungano kati ya Bara na Zanzibar. Kero zote hizo zikiondolewa tena nyingine hata si za kikatiba matatizo yatakuwa yameisha.”

Dk. Mwinyi, alisema kwa upande wa Tanzania Bara kero inayolalamikiwa ni kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri.

Alieleza ili kuondoa kero hiyo Bunge hilo linapaswa kutengeneza Katiba imara ya Jamhuri ya Muungano ambayo itaaisha vizuri mambo yote ya Muungano kikatiba.

“Tatizo hili litamalizwa kwa kuweka Constitution Suprimance (Ukuu wa Katiba), mambo haya yakirekebishwa amani itadumu, kutakuwapo na ustawi wa jamii na umoja wetu utadumu badala ya muundo wa serikali tatu ambao utatugawa na kuongeza mzigo wa gharama kwa wananchi” alisema.

 Alisema Katiba itakayoundwa inapaswa kuzingatia mambo makuu mawili, ambayo ni uwapo wa amani na kuleta ustawi wa jamii badala ya kuwagawa wananchi.
chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment