Wednesday, 19 November 2014

Stella: Nawachukia wanaume

Stella Makubi ndiyo kwanza ana umri wa miaka 26, lakini usimweleze habari ya kuishi na mwenza.

Akikumbuka madhila anayokumbana nayo, anasema hana hamu na wanaume kutokana na kile alichofanyiwa na mwanaume aliyewahi kuishi naye miaka.

Stella, anayeishi eneo la Msimba wilayani Kilosa, anasema mikasa ya maisha magumu anayopata sasa ilianza baada ya kukimbiwa na mwanaume baada ya kujifungua mtoto mlemavu wa viungo. Ifuatayo ni simulizi yake:

“Mtoto wangu anaitwa Meshack, baba yake alimkimbia baada ya kugundua ni mlemavu, amepooza mguu na mkono na niligundua kuwa ni mlemavu wa viungo baada ya mwaka mmoja. Pia hawezi kuongea mpaka sasa unavyomuona ana umri wa miaka nane hawezi kuita hata mama.


“Baada ya kugundua mtoto ni mlemavu mume wangu akaanza kunichukia na ndipo akakosa mapenzi ya mtoto na kukimbia. Ameondoka kijijini ameenda kuishi Morogoro mjini, na hatuna mawasiliano yoyote.

“Siku za nyuma mtoto alipozaliwa alikuwa anatoa huduma za mtoto, lakini tangu mtoto alivyogundulika ni mlemavu, sijaona msaada wake mpaka leo. Ninamtunza mtoto wangu mwenyewe, sijui wazazi wake wala ndugu zake.

“Tulikutana huku Msimba, na hakuwahi kunionyesha ndugu zake zaidi ni kaka yake mmoja ambaye siku za mwanzo nilimfuata na kumueleza, lakini alipuuzia na hakunipa msaada wowote. Sina msaada wowote zaidi ni mimi nahangaika na biashara yangu ya mkaa ndio inayonisaidia kumtunza mtoto wangu.”

Changamoto za malezi

Kwa kuwa ulemavu wa Meshack ni mkubwa, anahitaji uangalizi wa ziada na wa karibu. Anasema mara kwa mara anaumwa, hata shule ameshindwa kumpeleka kwa sababu hajimudu, wakati yeye analazimika kufanya kazi zaidi ili kumtimizia mahitaji muhimu.

Anachoshukuru Stella ni kuwa katika jamii anayoishi licha ya kukosa msaada wa kumwezesha kuishi na mtoto wake, majirani na ndugu katika hawamnyanyapai mwanawe, jambo linalompa faraja.

“Watoto wenzake wanacheza nae na wanajua kuwa mwenzao ni mlemavu, na kuna wakati wanamsaidia. Wameshamzoea kwa kuwa wameishi nae mwaka wa nane huu,’’ anaeleza.
chanzo mwananchi

No comments:

Post a Comment