Monday, 3 March 2014

Matusi, vijembe, vyatawala Bunge

Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba limeendelea kutawaliwa na vijembe na mipasho, huku baadhi ya wajumbe wakitambiana kujua misemo, mbinu na nahau na kuacha kujadili mambo ya msingi.
Mjadala wa upigaji wa kura wakati wa kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba, ndio ulioibua vijembe hivyo, huku wabunge wakigawanyika katika makundi mawili wanaotaka kura za wazi na wengine kura za siri.
Kila mjumbe aliyesimama alijitahidi kupambana na kuhakikisha anashinda,  jambo lililosababisha baadhi ya wajumbe kuchangia kwa hisia kali na maneno makali.
Said Alli Mubarak ndiye aliyeanza kuibua hoja ya upigaji kura za siri pamoja na kutaka wajumbe kufuata makundi ya walikotoka jambo lililosababisha wabunge kadhaa kulikataa suala hilo.
“Nataka tuanze kwa makubaliano hapa, maana vinginevyo hatutendeani haki. Sisi wengine kutoka Zanzibar tunajua namna ambavyo tumeonewa kwa kiasi kikubwa katika kipindi chote cha Muungano, hivyo lazima tukae na kujadiliana kwa pamoja,” alisema Mubarak.
Juma Duni Haji alizungumza kwa hisia kali akiwataka wajumbe kutoshabikia suala la kupiga kura kwa wazi na badala yake zipigwe kura za siri.
Mjumbe huyo alitolea mfano wa nchi za Uingereza na mataifa mengine,  akisema kuwa zilipiga kura kwa siri katika kufanikisha masuala yao.
Akijibu hoja hizo, Naibu Spika wa Bunge wa Jamhuri Job Ndugai, aliwataka wajumbe kuwa na staha katika mazungumzo, kwani ikitokea hivyo ukumbi hautatosha.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, hapatatosha hapa, maana mkianza kuzungumza habari za maonezi ya Muungano, ukumbi huu hautatosha, ni wazi kwamba tutagawana mbao humu ndani, msione sisi wengine tumenyamaza,” alisema Ndugai.
Katika majibu yake Profesa Maghembe alijikita zaidi kumjibu Duni kuhusu nchi ya Uingereza kutengeneza Katiba ya siri na kusema kuwa uelewa wa mjumbe huyo haukuwa mkubwa.
Profesa Maghembe alisema hakuna mahali ambapo Uingereza ilitengeneza Katiba ya siri kwa kuwa nchi hiyo haijawahi kuandika Katiba yake.
“Mtu mmoja hapa asubuhi kasema Katiba ya Uingereza ilipoandikwa watu walipiga kura ya siri, lakini mimi nafahamu hakuna Katiba ya Uingereza ambayo imeandikwa, watu hapa wana mazoea wakidhani kwamba wengine hawajui, wakati duniani kote hakuna kitu cha namna hiyo anadhani watu wote humu hawasomi au hawajui, Uingereza hakuna mtu aliyepiga kura ya siri utapigaje kura wakati hakuna katiba iliyoandikwa,”alisisitiza Maghembe.
Livingston Lusinde alisema ndani ya Bunge kuna watu waoga na wanafiki ambao waliisaliti na kuifuta nchi ya Tanganyika, lakini wameibuka upya kuidai.
Wabunge kuamua
Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba imeliacha jukumu la aina ya matumizi ya kura za siri yatumike au kura za wazi yafikiwe na Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa CostaMahalu alisema suala la aina gani ya kura itumike imewasumbua wakati wa kuijadili hivyo kufikia uamuzi huo.
Alisema iwe kura ya wazi au ya siri yote ni mchakato wa kidemokrasia na kati ya kura hizo hakuna inayomzuia mtu kupiga kura.
“Wajumbe walizungumzia namna zote za upigaji kura, kamati inakubali kuwa namna zote ni nzuri na kutokana hali hiyo Kamati imependekeza Bunge hili ndilo liamue ni aina gani ya kura itatumika,” alisema Profesa Mahalu.
Profesa Mahalu akizungumzia siwa alisema: “kutokana na gharama za siwa kuwa kubwa (Sh1 bilioni) tumependekeza iachwe kabisa kwa sababu za gharama, tutaulizwa na wananchi tumetumia gharama nyingi hivyo kifungu husika kitarekebishwa.”
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment