MAASKOFU wa Jumuiya ya Kikristo nchini (CCT), wametoa tamko na mapendekezo kadhaa kwa serikali ili iyafanyie kazi haraka iwezekanavyo kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Tamko hilo limetokana na kikao cha pamoja cha Halmashauri Kuu ya CCT hiyo kilichofanyika Juni mosi hadi mbili mwezi huu mjini Dodoma.
Akisoma tamko hilo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Peter Kitula, alisema wamefikia hatua ya kutoa tamko kutokana na kuona matukio kadhaa yakifanyika ndani ya jamii ambayo yanahitaji kukemewa na viongozi hao.
“Tulikaa Juni mosi hadi mbili mjini Dodoma ambapo maaskofu wote kwa pamoja tumekubaliana juu ya haya ambayo tunayatoa leo,” alisema Askofu Kitula.
Mauaji ya Nyamongo
Jopo hilo la maaskofu watano lililaani mauaji ya raia watano waliouawa katika eneo la Nyamongo na jeshi la polisi.
Katika tamko lao maaskofu hao walisema kuwa kumwagika kwa damu ya Watanzania hao siyo ishara nzuri hivyo hayo hayakubaliki.
Wameionya serikali juu ya uwekezaji katika madini, uvuvi, utalii ambapo uwekezaji huo wamedai kuwa umeshindwa kuwasaidia wananchi badala yake wamegeuka wageni ndani ya maeneo yao ya asili.
Maaskofu hao walisema kuwa hatua hiyo inawafanya wananchi kutokuwa na fursa ya kufanyakazi za kujikimu ndani ya maeneo hayo kutokana na kuonekana kama wezi na wavamizi, hali inayowafanya kuteswa hadi kuuawa.
Walisema wananchi wa maeneo hayo wanakabiliwa na changamoto kubwa na za hatari zikiwemo za uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wawekezaji hao.
Katika tamko lao hilo pia walionya mtindo wa serikali wa kutekeleza mambo kisirisiri hususan yale yanayogusa maslahi ya wananchi kama vile umilikaji wa ardhi, uvuvi, uchimbaji madini, utalii na uwindani pamoja na matumizi ya kodi ya wananchi mambo ambayo walidai kuwa hayakubaliki kwa Watanzania.
Kuandikwa kwa Katiba Mpya
CCT pia imempongeza Rais Kikwete kwa ujasiri wake wa kukubali kuridhia matakwa ya wananchi walio wengi ya kutaka kuandikwa kwa Katiba Mpya. Dira kubwa iwe kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa kwa kuzingatia amani, demokrasia, usawa na umoja wa kitaifa.
Pamoja na pongezi hizo, walisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ni jambo ambalo serikali halina budi kulisimamia na kuwaelimisha wananchi wote kwa usahihi na umakini.
Walishauri kuwa zoezi la ukusanywaji wa maoni halina budi kufanywa na chombo huru na lisiharakishwe na lisichelewe.
Kadhalika wameshauri uundwaji wake uwe umekamilika mapema ndani ya muda wa kadri kabla ya kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Tiba ya Babu Loliondo
Aidha CCT imezungumzia tiba ya Loliondo ikisema kuwa serikali haina budi kutoa ushirikiano zaidi kwa wadau hao na kuishauri isimamie utunzaji wa mazingira ili miti na mimea mingine yenye vyanzo vya tiba asilia istawi na kupatikana muda wote.
Rushwa na Ufisadi
Katika maelezo yao, maovu yanayotajwa kila siku ikiwa ni pamoja na rushwa, ufisadi na uporaji wa raslimali za taifa walionya kuwa yasifanyiwe mzaha ili kuepusha kuleta maangamizi kwa raia wasio na hatia.
Katika kuepusha hali hiyo, maaskofu hao walionya viongozi wanaotoa kauli zenye maneno matamu yenye lengo la kuwapotosha wananchi kwa lengo lao binafsi au kuwachanganya wananchi na kuleta migogoro.
Jopo hilo liliongeza kwamba suala la Mahakama ya Kadhi ni jambo zuri, lakini waachiwe Waislamu wenyewe pasipo serikali kuliingilia.
Aidha walionya juu ya kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo tatizo la nishati ya umeme nchini.
Alipoulizwa juu ya kikao cha Bunge kinachotarajiwa kuanza leo, Mwenyekiti wa CCT, alisema Bunge linaloanza leo mjini Dodoma halina budi kuangalia juu ya kuwapatia nafuu ya maisha wananchi badala ya kujali maslahi ya wachache na wenye nazo.
Mwenyekiti huyo alisema bajeti hiyo inatakiwa kuongeza mishahara kwa wafanyakazi, huku ikitoa kipaumbele kwenye elimu, afya na kushauri kuwepo na madawa ya kutosha na yatolewe bila upendeleo.
No comments:
Post a Comment