JUMLA ya wananchi 835 toka katika kaya 150 za kijiji cha Mosongo wilaya ya Serengeti, mkoa wa Mara, hawana sehemu ya kukaa baada ya maeneo yao kuvamiwa na watu wanaosemekana wanatoka katika nchi jirani ya Kenya.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dare s Salaam jana, wananchi hao kupitia kwa wawakilishi wao, Wilson Nyamchabha, Maro Nyamhanga, Daudi Noeli na Prackiseda Mwita, huku wakiwa na barua waliyomwandikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi walisema chanzo cha wao kuondolewa katika makazi yao kilianza mwaka 2009.
Walidai kuwa Aprili 17, 2009 kijiji chao kilivamiwa na wahamiaji haramu wa kabila la Wakurya toka katika ukoo wa Nyabasi waliotoka nchi jirani ya Kenya na wengine kutoka wilaya ya Tarime na kusababisha mauaji kwa baadhi ya wanakijiji cha Mosongo.
Wakazi hao wanaotoka katika kabila la Wangoreme, Wanyiramba, Wasukuma, Waikizu na Waikoma walidai kuwa genge hilo la wavamizi linapewa nguvu ya kufanya vitendo vyao na uongozi wa wilaya chini ya mkuu wa wilaya ya Serengeti, Luteni mstaafu Edward Ole Lenga
“Tumeshatoa taarifa hizi wilayani na mkoani lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya kundi hilo na kutuwezesha sisi kurudi katika makazi yetu, mkuu wa wilaya ndugu Edward Ole Lenga amechangia kwa kiasi kikubwa watu kupoteza maisha na makazi yao kwa kuwakingia kifua wanaofanya vitendo hivyo,” alisema Nyamchabha.
Aidha wakazi hao wa Mosongo walimtuhumu mkuu wa wilaya ya Serengeti kuwa anawaweka rumande watu wanaoonekana kufuatilia suala hilo na kukataza kupata dhamana pasipo kuwaeleza sababu za msingi za kuzuiliwa kwao.
Wakazi hao walisema wanahofia kurudi katika maeneo yao kutokana na vitendo vilivyojitokeza kwa baadhi yao kuuawa walipojaribu kurudi katika eneo hilo; walimtaja aliyekutwa na kadhia hiyo kuwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa kijiji hicho Noel Mathayo.
Mbunge wa jimbo la Serengeti Dk. Kebwe Kebwe, alipopigiwa simu alisema yeye yuko Dodoma na hawezi kulizungumzia hilo mpaka atakapokutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Serengeti, Edward Ole Lenga, alikanusha kuwepo na wakazi waliobomolewa nyumba zao, na kuwashangaa hao waliolifikisha suala hilo kwenye vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment