MAHAKAMA ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa jana imemhukumu kwenda jela miaka sita, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Pomerini wilaya ya Kilolo mkoani hapa, Michael Ngilangwa, ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Njombe kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Martha Mpaze baada ya mwalimu huyo kupatikana na hatia katika mashtaka mawili yaliyokuwa yakimkabili katika kesi iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Tushwa Tanzania (Takukuru) mkoa wa Iringa.
Alisema kuwa mahakama hiyo imeridhia na ushahidi uliotolewa pamoja na vielelezo
vilivyowasilishwa mahakani hapo ili liwe fundisho kwa wengine mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi yake.
Alisema katika kosa la kwanza mwalimu huyo anadaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake huyo jina (limehifadhiwa) ili kumsaidia masomo ambapo adhabu yake ni kulipa faini ya shilingi laki tano ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, na kosa la pili ni kutaka kumbaka mwanafunzi huyo ambapo mahakama hiyo inamhukumu kwenda jela miaka mitano
Hakimu Mpaze alisema mahakama imetoa hukumu hiyo kwa kuzingatia
maombi ya pande zote mbili, yaani wa mashtaka na mshtakiwa na kwamba
milango ya dhamana iko wazi iwapo mshtakiwa hajaridhika na uamuzi huo
wa mahakama.
Awali kabla ya hukumu hiyo mwendesha mashtaka wa TAKUKURU mkoa wa Iringa, Nitume Mizizi,
aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa kuwa
kitendo alichokifanya si cha kiungwana na hasa ikizingatiwa aliacha
majukumu yake ya kazi na kuamua kumuomba rushwa ya ngono mwanafunzi
wake na kujaribu kumbaka.
Kwa upande wake mshtakiwa huyo aliiomba mahakama impunguzie mzigo wa
adhabu, kwa kuwa ana majukumu makubwa ya kifamilia, kwani anasomesha
wanafunzi wanne, wawili wakiwa yatima na pia anamhudumia mama yake
mzazi mwenye umri wa miaka 82.
Mwalimu Ngilangwa ambaye pia ni mchungaji wa Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKT) dayosisi ya Njombe alitenda kosa hilo la kuomba rushwa ya ngono na kujaribu kumbaka
mwanafunzi wake huyo wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 14,
kati ya Agosti 10 na 11, mwaka 2011, katika nyumba ya kulala wageni ya
Wihanzi iliyoko mjini Iringa, kinyume na kifungu namba 25 cha sheria
ya kupambana na kuzuia rushwa ya mwaka 2007.
No comments:
Post a Comment