KOCHA wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Jan Poulsen, aliwataja nyota 23 wa kucheza na Msumbiji kwenye kampeni ya kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwakani nchini Afrika Kusini, huku nyota wa kimataifa, Mbwana Samatta na Henry Joseph wakiachwa.
Nyota wengine wa kimataifa waliochwa ni Athuman Machuppa wa Vassuland IF, Sweden na Dany Mrwanda.
Kabla ya kuivaa Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hapo Februari 29, Stars itacheza mechi moja ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya DR Congo, itakayopigwa Februari 23, kwenye Uwanja wa Taifa.
Nyota walioitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Februari 20, ni viungo Jonas Gerald kutoka Simba na Salum Aboubakar wa Azam FC.
Kikosi kamili kinaundwa na makipa: Shabani Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam).
Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Juma Jabu (Simba), Stephen Mwasyika (Yanga) na Kelvin Yondani (Simba).
Viungo ni Jonas Gerard (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Shomari Kapombe (Simba), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Abdi Kassim (Azam).
Washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam), Nizar Khalfan (Philadelphia Union, Marekani), Mrisho Ngasa (Azam), Ally Badru Ally (Canal Suez, Misri), Uhuru Selemani (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).
Akizungumza wakati wa kutangaza majina hayo, Poulsen alisema kuachwa kwa Samatta anayekipiga TP Mazembe ya DR Congo, ni kushindwa kudhihirisha uwezo licha ya kupewa nafasi ya kufanya hivyo kwenye kuwania tiketi ya Kombe la Mataifa Afrika 2012.
Poulsen amewapongeza Kapombe na John Bocco kwa kutunza viwango vyao tofauti na wengine wakiwamo wakongwe ambao uchezaji wao umekuwa ukipanda na kushuka.
Mbali ya nyota wa kimataifa, wengine waliotemwa safari hii ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita, Nurdin Bakari wote wa Yanga na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa Azam.
Poulsen, aliyetumia muda mwingi kuchambua uwezo wa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, alisema, anavutiwa na uwezo wa nahodha wake, Nsajigwa, akisema ni aina ya mchezaji mwenye uwezo mkubwa ndani na nje ya uwanja, hivyo ni mtu muhimu katika kikosi hicho.
Alisema anaamini timu hiyo itafanya vizuri dhidi ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na mechi ya marudiano mjini Maputo.
No comments:
Post a Comment