Thursday, 3 May 2012

'House Girl' Upanga adaiwa kuiba mali ya mil 20/-!!

MFANYAKAZI wa ndani, Mary Msikwa amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na shitaka la wizi wa mali za Sh milioni 20. 

Msikwa (28) alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa shitaka linalomkabili mbele ya Hakimu Wilberforce Luhwago. 

Wakili wa Serikali Sakina Sinda alida kuwa, Machi 3, mwaka huu saa 2:00 asubuhi katika mtaa wa Olympio eneo la Upanga, mshitakiwa aliiba mapambo ya dhahabu, fedha , nguo mbalimbali na vifaa vingine vya jikoni vyote vikiwa na thamani hiyo mali ya Yande Benedictor. 

Mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo na kurudishwa rumande kwa kukosa wadhamini, kesi hiyo itatajwa tena Mei 17 mwaka huu. 

Katika hatua nyingine, dereva Musa Ramadhani (34) alifikishwa mahakamani hapo kwa shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. 

Akisoma shitaka mbele ya Hakimu Karim Mushi Wakili wa Serikali Alice Mtulo alidai kuwa, Aprili 16 mwaka huu saa 7:00 mchana katika mtaa wa Agrey, Ramadhani alijipatia Sh milioni 5.25 kutoka kwa Cheha Soifoine kwa madai ya kwenda kumnunulia hiliki lakini badala yake alizitumia fedha hizo wa matumizi yake binafsi. 

Mshitakiwa alikana shitaka hilo na kurudishwa rumande hadi Mei 15 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
                         
                         chanzo ni habari leo

No comments:

Post a Comment