Habari kutoka kata za Kilema Kusini, Kilema Kaskazini na Marangu zinadai kuwa mtandao wa majambazi hao wapatao 30, umekuwa ukilipiza kisasi kwa wananchi wanaojitokeza kutoa ushahidi polisi.
Wananchi hao wamependekeza kutumika kwa sheria ya kuwaweka kizuizini watuhumiwa, ili kuepuka uwezekano wa kuua watu.
Habari zilizozagaa katika Kijiji cha Makami Juu, zilidai kuwa usiku wa Septemba 11 mwaka huu, majambazi walimvamia mfanyabiashara, Respich Ngowi na kumuua kwa kumdunga sindano ya sumu.
“Waliiba kila kitu na wakamdunga sindano ya sumu, watu hawakuthubutu kutoka nje ya nyumba wakihofia kukatwa mapanga na kufuatiliwa na mtandao huo wa majambazi,”alidai mwananchi mmoja.
Wananchi hao walidai kuwa uchunguzi wa mwili wa marehemu uliofanywa na madaktari, ulithibitisha kuwa mfanyabiashara huyo alichomwa sindano mbili za sumu.
Mtandao huo ndio unaotuhumiwa kuilipua kwa petrol, nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiraracha, Andrew Lekule na kuteketeza mkewe na mtoto wao mdogo wa umri wa miaka mitano.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Kitowo huko Kilema ,alidai kuwa mtandao huo ni kama umejitangazia “uhuru” kwa sababu unafanya uhalifu wakati wowote wanapojisikia kufanya hivyo.
“Ukiuza nguruwe wanakufuata usiku na hata ukiuza mti wako wanakuja na mapanga wanataka pesa za mauzo. Hali si nzuri hata kidogo karibu kata nzima ya Kilema Kaskazini,”alidai.
Hata hivyo mkazi wa Kijiji cha Ruwa alilidokeza gazeti hili kuwa pamoja na jitihada za polisi kukamata washukiwa lakini wananchi hawataki kutoa ushirikiano ikiwamo kuwatambua wahalifu.
“Tatizo hapa ni wananchi ambao hawana mwamko wa ulinzi shirikishi, yaani mtu anavamia nyumbani na anapiga yowe la kuomba msaada, lakini hakuna jirani anayetoka na kutoa msaada”alidai.
Mwananchi huyo ambaye naye hakupenda jina lake litajwe, alidai kuwa kama wananchi wangekuwa na umoja, wangeweza kusambaratisha mtandao huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kuwapo kwa matukio ya ujambazi, lakini alisema tatizo ni wananchi wanaokataa kuwatambua washukiwa wala kutoa ushahidi.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, hivi karibuni alikwenda katika Kijiji cha Kitowo na kukabidhiwa majina ya washukiwa lakini alipowauliza waliompa majina kama wako tayari kutoa ushahidi, walikataa.
Alisema hivi karibuni waliwakamata watuhumiwa wanane lakini ilibidi watumie utaratibu wa kisheria unaojulikana kama “Binding Over” ambapo mahakama iliwaweka chini ya uangalizi wa miaka miwili.
Katika kipindi hicho, watuhumiwa hao hawatakiwi kufanya kosa lolote la jinai.
Kamanda Boaz alisema kutokana na mazingira ya wananchi kutokuwa na mwamko wa ulinzi shirikishi, Jeshi la Polisi limeanza mchakato wa kuzunguka katika vijiji vyote vya kata hizo, ili kutoa elimu hiyo.
Kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Ngowi anayedaiwa kudungwa sindano ya sumu, alisema japo wananchi wamejenga hisia hizo lakini msema kweli ni taarifa ya daktari.
Kamanda Boaz alisema ofisi yake itafuatilia taarifa hiyo ili kujiridhisha kuhusu sababu za kifo hicho.Akizungumza na gazeti hili, Mbunge wa Vunjo, Agustino Mrema (TLP), amelitaka Jeshi la Polisi kujibu mapigo, vinginevyo wananchi watapata hisia kuwa limezidiwa nguvu na majambazi hao.
“Hali ya uhalifu inapanda Kilema na Marangu na polisi wasipojibu mapigo haraka, hali itakuwa mbaya sana na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kuusambaratisha mtandao huo,”alisema.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment