KESI ya viongozi wa Uamsho kupinga kufungwa dhamana yao na kupewa huduma duni gerezani imetupwa na Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Mkusa Isack Sepetu, jana kutokana na kesi hiyo kufunguliwa kinyume na sheria.
Viongozi hao walifungua kesi hiyo Novemba 8 wakitaka Mahakama Kuu kufanya mapitio ya maamuzi ya awali yaliyotolewa katika kesi ya msingi na Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Kazi.
Viongozi hao wa Jumuiya ya Uamsho wakiwakilishwa na Wakili Abdalla Juma Mohamed, walikuwa wakipinga hatua ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee kufunga dhamana yao kwa kutumia kifungu cha 3 (d) cha sheria ya Usalama wa Taifa sura ya 47 ya mwaka 2002.
Aidha viongozi hao walikuwa wakipinga kitendo cha uongozi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kuwanyima haki ya kula chakula kutoka nyumbani, kufanya ibada pamoja, kubadilisha nguo, kusoma vitabu vya dini (Koran), na kufungiwa kila mshitakiwa katika selo yake kwa muda wa saa 24 pamoja na kunyolewa ndevu.
Akitoa huku hiyo, Jaji Mkusa alisema kwamba kesi hiyo ilifunguliwa kinyume na kifungu cha 4 cha sheria ya mawakili na wanasheria sura ya 28 ya sheria ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa sheria, hati ya kiapo ilitakiwa kuwa na tarehe na jina la mtu aliyekula kiapo kwa niaba ya viongozi wa Uamsho mambo ambayo hayakuzingatiwa kabla ya kufunguliwa kwa kesi.
Jaji Mkusa alisema kwamba pamoja na hati za kiapo kutayarishwa na wakili mwenye uzoefu, Abdalla Juma Mohammed, lakini hakuzingatia taratibu za kisheria za kufungua kesi kama hiyo.
Hata hivyo, aliwataka wanasheria kuwa makini wanapowasilisha maombi kama hayo au nyaraka kwa kuangalia kama maombi yao yamekidhi matakwa ya kisheria.
Pia katika kesi hiyo, Jaji Mkusa ametupilia mbali pingamizi dhidi ya kesi ya viongozi wa Uamsho ambayo iliwasilishwa na wanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar.
Wanasheria wa serikali; Ramadhan Nasib na Raya Mselem walidai kwamba kesi ya viongozi wa Uamsho imefunguliwa kinyume na sheria kwa sababu hati ya kiapo haikuwa na jina la wakili aliyekula kiapo kwa niaba ya wateja wake pamoja na tarehe ya kiapo hicho.
Katika hukumu yake, Jaji Mkusa, alisema wanasheria wa serikali pia wamefungua pingamizi hiyo kinyume na kifungu cha 4 sura 28 ya sheria ya mawakili na wanasheria Zanzibar.
Jaji Mkusa alisema kwamba nyaraka za pingamizi zilitakiwa kuonyesha jina la mtu aliyetayarisha pingamizi hiyo kabla ya kuwasilishwa mbele ya Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Hata hivyo, Jaji Mkusa ameutaka uongozi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kuhakikisha wanatenda haki dhidi ya viongozi wa Uamsho kwa kuwapatia haki ya huduma wakiwa katika gereza la Kinua miguu Mjini Zanzibar.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya Chuo cha Mafunzo namba 3 ya mwaka 2007 viongozi wa Uamsho wanastahili kupatiwa huduma sawa na mahabusu wengine.
Kwa upande wake, Wakili Salim Toufiq, alisema kwamba wateja wake tayari wameanza kupatiwa huduma zote, isipokuwa wamekuwa wakinyimwa haki ya kukutana na ndugu na jamaa.
Viongozi waliofungua kesi ya kupinga kufungwa dhamana na kunyimwa huduma bora ni Sheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, Azzani Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakari Suleiman na Ghalib Ahmada Omar.
Aidha, Jaji Mkusa alisema kesi ya msingi inayowakabili viongozi wa Uamsho ya tuhuma za uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa taifa imepangwa kutajwa tena Januari 3 mwakani.
chanzo:mwanachi
No comments:
Post a Comment