Thursday, 24 January 2013

Kiwanda cha Mchina chaua wanne mjini Kibaha

Watu wanne wamefariki dunia katika mlipuko unaodaiwa kuwa ni wa bomu ambao umetokea kwenye kiwanda cha Hong Yu Steel cha kuyeyusha vyuma chakavu kilichopo Zogoani, katika mji wa Kibaha.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema tukio hilo lilitokea juzi na kwamba ni mlipuko uliosababishwa na ajali ya kawaida.

Alisema tayari mabaki ya vyuma vilivyolipuka yamepelekwa kwa wataalam wa milipuko kwa uchunguzi zaidi na kwamba taarifa zitatolewa baadaye.

Matei alisema mlipuko huo ulitokea wakati uyeyushaji wa vyuma ukiendelea na kwamba hiyo ni ajali ya kawaida.

“Hatuwezi kusema sasa kwamba ni bomu kwa sababu kwanza madhara yametokea tu kwa binadamu, bomu lingeweza kuvunja kuta na paa. 


Tunasubiri majibu ya wataalam ambao wanachunguza tukio hili,” alisema.

Alisema jana Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, ilifanya ziara kiwandani hapo  kujionea hali halisi na kujiridhisha kwamba kiwanda kisitishe shughuli zake kwa muda.

Alisema tangu ajali hiyo ilipotokea juzi, menejimenti ya kiwanda ilitangaza kusimamisha shughuli zake kwa muda wa siku tatu na kwamba jana imekubaliwa kwamba kisimamishe uzalishaji kwa muda mrefu 
zaidi. 
Kamanda Matei alisema katika ajali hiyo, watu wanne walifariki ambao ni Watanzania watatu na raia mmoja kutoka China. 

Kamanda Matei aliwataja waliofariki kuwa ni Kassim Mtulia (26), George Manumbu (25), Mwinjuma Hussein (25) wote Watanzania pamoja na Yu Huafing (28) raia wa China.

Alisema katika mlipuko huo watu kadhaa walijeruhiwa na kutibiwa Hospitali ya Tumbi. 
Kati ya waliojeruhiwa, mmoja kati yao bado yuko hospitali na hali yake inaendelea vizuri huku wengine wakiwa wameruhusiwa.

Hili ni tukio la pili kutokea baada ya lile la Oktoba mwaka jana wakati mlipuko kama huo ulipotokea Mikocheni, jijini Dar es Salaam eneo la kwa Warioba karibu na Kanisa Katoliki la Mtakatifu Martha baada ya vijana waliokuwa wakiuza nyaya aina ya kopa kama vyuma chakavu kulipuka na kusababisha majeruhi kwa msichana mmoja na wengine kunusurika.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment