Mkurugenzi mtendaji wa umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC)Abubakar Karsan ameitembelea familia ya marehemu Daudi Mwangosi ambae alikuwa mwandishi wa Chanel Ten mkoa wa Iringa na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) na kuahidi kuisaidia familia hiyo kwa kuanisha mradi wa kudumu.
Akizungumza na mjane huyo nyumbani kwake eneo la Kihesa Kilolo mjini Iringa leo Karsan mbali ya kumpa pole kwa kifo cha Mwangosi bado alisema kuwa UTPC itaendelea kuwa jirani na mjane huyo kwa kumtafutia shughuli ya kudumu ya kufanya ili kumuongezea kipato.
Karsan alisema kuwa lengo la ziara yake mkoani Iringa ilikuwa ni kukutana na mjane huyo ili kujua ni shughuli ipi ya kiuchumi anaweza kuifanya na kwa kauli yake mjane huyo wa Mwangosi amechagua kufanya kazi ya ufugaji wa kuku wa kisasa .
Hivyo alisema kutokana na uamuzi wa mjane huyo Mwangosi kuchagua kuifanya kazi hiyo wao kama UTPC katika kuendelea kumuenzi marehemu Mwangosi ambae alikuwa ni kiongozi wa IPC na UTPC kama walezi wa vilabu vya waandishi wa habari nchini watahakikisha mjane huyo anasomeshwa masomo ya ujasiriamali hasa kwa kuzingatia shughuli hiyo ya ufugaji kuku ambayo anataka kuifanya kabla ya kumpa mtaji wa kuendesha ufugaji.
Wakati huo huo UTPC imemshauri mjane huyo kwa sasa kutozungumza chochote na vyombo vya habari bila kuwasiliana na UTPC ili kuepuka mkanganyiko wa taarifa kama ilivyopata kujitokeza hivi karibuni.
Karsan amesema kuwa ili kuendelea kulishughulikia suala hilo la mauwaji ya Mwangosi ni vema kukawa na utaratibu mzuri wa kitaalam zaidi katika kutoa taarifa na kuwa mjane huyo kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari basi kuweza kuwasiliana na UTPC ili kujua ni nini ambacho anataka kukisema.
"UTPC itaendelea kuwa karibu na wewe na familia kutokana na Mwangosi kuwa ni mwanachama wetu na katika kuendelea kuuenzi mchango wake katika tasnia ya habari mkutano mkuu wa UTPC kuanzia mwaka huu utakuwa ukifanyika Septemba 2 siku ambayo Mwangosi aliuwawa .....ila pia tutaendelea kukusaidia kuwa na shughuli yenye kipato ya kufanya ....lakini wakati suala zima la mauwaji ya Mwagosi linaendelea kufanyiwa kazi na vyombo vya usalama na UTPC tunaendelea kulishughulikia na tunaomba kwa sasa kutozungumza chochote bila kuwasiliana nasi"
UTPC kupitia vilabu vya wanahabari nchini katika msiba huo wa Mwangosi ilitoa ushirikiano mkubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuchangia shughuli mbali mbali za mazishi na pesa ya kumsaidia mjane huyo zaidi ya mamilioni ya shilingi .
chanzo:.globalpublishers
No comments:
Post a Comment