Friday, 25 January 2013

Vipindi vya mapenzi mchana! Serikali iko wapi?????


KUNA baadhi ya matukio yamekuwa yakitangazwa kupitia baadhi ya vyombo vya habari, ambayo kwa kweli msingi wake ni kuipotosha jamii.
Matukio hayo yamekuwa yakitangazwa na baadhi ya vituo vya redio, ambazo wakati mwingine unaweza kujiuliza ni maadili gani ya kazi wamejifunza wahusika katika vyuo vya uandishi wa habari walivyosoma.
Baadhi ya vipindi vya vituo hivyo, vimekuwa kero kutokana kutojali matangazo yao yanawalenga wasikilizaji wa rika gani.
Kwa kawaida, kuna vipindi ambavyo havipaswi kusikilizwa au kuonwa na watoto, ndiyo maana vinatakiwa kutangazwa usiku wakati watoto wakiwa wamelala.
Lakini kutokana na mfumo wa utandawazi, siku hizi baadhi ya vituo hivyo havijali tena maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Hali hiyo ya kutangaza vipindi bila kujali utamaduni wa Watanzania, imekuwa ikilaaniwa na baadhi ya wazazi, ingawa vituo hivyo haviko tayari kubadilika hadi sasa.
Matangazo yanayolalamikiwa na baadhi ya wananchi ni kuhusiana na mazungumzo ya matendo ya mapenzi, ambayo kiukweli siwezi kuyataja hapa.
Mambo ya mapenzi kwa kawaida yana muda wake na kwa siri, hivyo ni ajabu kusikia baadhi ya vituo hivyo vya redio kuyatangaza hadharani.
Vipindi hivyo vimekuwa vikitaja baadhi ya matendo yanayofanywa na watu wa jinsia mbili tofauti katika mapenzi, mchana kweupe!
Chuki kutoka kwa watu wasiopendelea utaratibu huo, hujitokeza zaidi kwenye vyombo vya usafiri wa umma kama vile daladala, ambako hupanda watu wa rika mbalimbali ikiwemo watoto wadogo.
Kuna vitu vimekuwa vikizungumzwa, kiukweli havipaswi kuzungumzwa katika mazingira kama hayo ya mchanganyiko wa watu.
Ukiangalia vipindi hivyo, havina mafundisho yoyote zaidi kuwapotosha watoto wanaovisikiliza.
Niliwahi kudadisi, labda inakuwaje vipindi hivyo vimekuwa vikiachiwa hewani bila kuchujwa, lakini inaelezwa kuwa huu ni wakati wa soko huria, hivyo kila kinachofanywa, lengo ni biashara zaidi.
Aidha, wapo wanaodhani kuwa, mapenzi siku hizi yamekuwa burudani, hivyo katika vituo hivyo matangazo hayo ni moja ya njia ya kuwavutia wateja zaidi. Vipindi hivyo vinazidi kuongezeka kila kukicha.
Waganga wa jadi pia nao hujitokeza kununua vipindi kwa ajili ya kutangaza biashara zao za dawa za kuimarisha mapenzi na kudumisha ndoa.

Safu hii ina ushahidi wa baadhi ya vipindi hivyo vinavyotangazwa majira ya saa 5:00 asubuhi, ndio maana nazungumza kwa kujiamini bila ya kujing’atang’ata.
Sitaki kuyataja hayo yanayozungumzwa katika vipindi hivyo, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa nimeshiriki katika kile kinachopingwa na baadhi ya watu na ninachotaka tuwekane sawa.
Labda kwa pamoja, naomba tujiulize, hivi ni kweli kwamba vipindi hivyo vya ushauri wa kimapenzi kupitia redio vinatoa mafunzo kweli?
Kiukweli, binafsi sitaki kuamini hivyo, ingawa siko tayari kuzungumzia utashi wa mtu mwingine, bali matangazo hayo hayawezi kumsaidia mtu ambaye tayari hulka yake imekwishajengeka hivyo, zaidi… ni kuiharibu jamii ya watoto wanaotarajiwa kuwa wazazi hapo baadaye.
Safu hii inaona, kuna ulazima kwa Idara ya Habari (Maelezo) kuwa makini katika kufuatilia vipindi hivyo ambavyo naamini vinaleta athari mbaya.
Kama Idara hiyo haitaki tuwekane sawa katika kuvifuatilia vyombo hivyo vya habari, kwa kujiamulia vipindi wanavyotaka kwa lengo tu la maslahi, kiukweli nchi hii itajikuta ikilea jamii ya watu wachafu kimaadili.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment