Thursday, 28 February 2013

Hatuna mpango wa kuwasaidia waliofeli kidato cha lV-Mulugo


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema wizara haina mpango wowote kwa sasa kuhusiana na wanafunzi waliofeli kidato cha nne mpaka pale Tume itakapomaliza kufanya kazi yake ndipo itaamua nini cha kufanya.
 
Mulugo aliliambia NIPASHE kuwa wizara inasubiri Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, imalize kufanya kazi yake, ndipo itatoa uamuzi nini kifanyike juu ya wanafunzi hao.
 
“Kwa sasa siwezi nikasema chochote kwani tume imeundwa ili kulifanyia kazi jambo hilo, hivyo tunasubiri wamalize kufanya kazi yao ndipo tutatoa kauli ya nini kifanye juu ya wanafunzi walio feli kama ni kurudia tena mtihani au la,” alisema Mulugo.
 
Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa wizara yake inazungumziaje juu ya mpango wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu kuandaa mafunzo ya kozi ya muda mfupi kwa vijana wote waliofeli mkoani humo ili kuwapima kama wapo wanaaoweza kusaidiwa kuendelea na elimu ya cheti.
 
Msambatavangu alitoa uamuzi huo baada ya makubaliano yake na baadhi ya vyuo vikuu kama Chuo Kikuu cha Tumaini (IUCO) na Chuo kikuu cha Ruaha (Ruco) na kukubaliana kutoa mafunzo hayo yatakayo anza Machi mwaka huu. 
 
Mulogo alisema kuwa ni wazo lenye mpango mzuri wa kuwasaidia vijana wengi ambao ni kama wamekumbwa na tatizo kwa sasa, hivyo anacho kifanya Mwenyekiti huyo hakina madhara yoyote  na anafanya kama raia mwema aliyeguswa na matokeo hayo
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment