UONGOZI wa Clouds Media Group kupitia Mkurugenzi wao wa Utafiti na Matukio, Ruge Mutahaba, umemtaka msanii wa Bongo Fleva, Judith Wambura, ‘Lady Jaydee’ ajipange na kupokea changamoto badala ya kutafuta mahali pa kuegemea kwa kusambaza matusi kwao.
Clouds Media, jana walifungua mdomo kwa mara ya kwanza tangu Jaydee alipokuwa akiwarushia makombora kwa madai kuwa wamemfanyia mambo mabaya na kutaka kumuangamiza kimaendeleo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Mutahaba alisema Jaydee amekuwa akilalamikia mambo mawili ambayo ni bendi ya Skylight na matangazo yake yaliyoshindwa kurushwa hewani japo alilipia sh 240,000.
Alisema suala hilo walilimaliza baada ya kumueleza kuwa redio yao haiwezi kukataa matangazo, kwa kuwa ndiyo yanayowafanya waendelee kuwa kinara katika suala zima la kuiendesha Clouds FM.
“Nilimwambia kamwe hatuwezi kukataa matangazo na kama kuna lolote limefanyika, basi ni kwa bahati mbaya, ukizingatia kuwa tayari alishafanya kazi nyingi pamoja na kupewa urahisi kwenye kazi zake kwa kupitia Clouds FM.
“Pamoja na yote hayo, bado matusi na kejeli yaliendelea hasa katika mitandao ya kijamii, jambo lililotufanya tuamue sasa kujibu japo hapo kabla tuliamua kubaki kimya kwa ajili ya kulinda hadhi ya kazi zetu,” alisema.
Kuhusu shutuma za kuitangaza zaidi Skylight, Ruge alisema, bendi hiyo si mali ya Joseph Kusaga, mkurugenzi wao wala yeye, kama madai hayo yanavyotolewa bila kufanya utafiti, isipokuwa ni mali ya Sebastian Ndege.
“Kama kuna mvutano kati ya Machozi Bendi na Skylight, basi ni wa kibiashara, maana wote wanalipa fedha za matangazo na kama chanzo ni Jaydee kuporwa wanamuziki wake, hilo si jambo geni kwenye muziki.
Dada yangu Asha Baraka asingekuwa makini angelia sana, maana kila bendi inayoanzishwa au kuendeshwa lazima ichukue wanamuziki kutoka kwake, ukizingatia kuwa ni jambo la kawaida, hivyo tunamuomba Jaydee atumie busara katika hili pamoja na kuumiza kichwa kupokea ushindani na changamoto kama hizo za kuchukuliwa wanamuziki,” aliongeza Ruge.
Aidha, Ruge alisema Clouds FM ni redio ya watu binafsi, hivyo ina utaratibu wake katika utendaji wa kazi, ikiwamo kuchagua nyimbo au kuacha kupiga kama kuna mtu amekwenda kinyume, hasa wale wanaopita nje na kuanza kuwatusi na kuwakejeli bila kukumbuka fadhila walizofanyiwa kabla ya kuwa maarufu.
Pia alisema Clouds FM ipo tayari kufanya majadiliano ya wazi na mtu yeyote mwenye hisia tofauti juu yao, huku ikiwataka wasanii waongeze bidii katika kazi zao ili wasimlaumu mtu wanapoanguka na kuwapisha wengine, maana muziki unaonekana ni wa kupokezana vijiti.
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment