Tuesday, 7 May 2013

Ugaidi Arusha: 10 mbaroni

Watuhumiwa 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, watano wakiwa raia wa Saud Arabia kufuatia mlipuko wa bomu lililotupwa na kulipuka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti, mjini Arusha juzi na kusababisha vifo vya watu watatu.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ni bomu. Uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na wataalamu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Waliokufa wametajwa kuwa ni Regina Longino Kurusei (45), James Gabriel (16) na mwingine jina lake halikuweza kutambulika.

Habari zilizopatikana jana zinasema mtu wa tatu aliyekufa ambaye hajatambulika ni yule aliyechukuliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal kwa ajili ya kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, ambaye alifariki jana akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).


Kufuatia tukio hilo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kwa kushirikiana na wakuu wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wameunda kikosi kazi maalumu kuchunguza tukio hilo.

Akitoa kauli ya Serikali bungeni jana kuhusu mlipuko huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kutokana na uzito wa tukio hilo, Makamu wa Rais, Dk. Ghalib Bilal, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, walikwenda Arusha na kutembelea eneo la tukio na majeruhi na kuelekeza hatua za ziada kuchukuliwa.

Alisema miongoni mwa waliokamatwa ni Victor Calisti Ambrose (20) ambaye ni dereva wa bodaboda mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha, anayetuhumiwa kurusha bomu hilo. 

Akitoa taarifa ya tukio hilo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, jana alisema raia wa Saud Arabia waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo waliingia nchini Mei 4 mwaka huu kupitia KIA na walikamatiwa katika mpaka wa Namanga wakijaribu  kutoroka kupitia nchi jirani ya Kenya.

Alisema watuhumiwa hao hawajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, hivyo polisi wanatafuta mkalimani ili waweze kuhojiwa kwa kutumia lugha ya Kiarabu.

Kuhusu raia wa Kenya, alisema anasadikiwa kuwasaidia raia hao wa Saud Arabia kuingia nchini.

Akizungumza bungeni jana, Dk. Nchimbi alisema katika tukio hilo watu 59 walijeruhiwa na watatu kati yao ni mahututi. Majeruhi 38 walikimbizwa hospitali ya Mount Meru, 16 walikimbizwa hospitali ya St. Elizabeth kwa Father Babu na mmoja alipelekwa hospitali ya Dk. Wanjara, Mianzini. 

Hata hivyo, alisema viongozi wa dini na serikali waliohudhuria ibada hiyo hawakupata madhara. 

Alisema baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha waliimarisha ulinzi kwa kuongeza idadi ya askari katika eneo hilo. Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulogo, walifika eneo la tukio na kufanya tathmini ya hali ilivyo na kuelekeza hatua za kuchukuliwa.

“Sina shaka kuwa shambulio la Arusha ni sehemu ya mikakati miovu. Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa serikali haitavumilia hata kidogo mbegu za chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na tutachukua hatua kali bila huruma kuzikandamiza njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu,” alisema.

Alisema pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao, yeye na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wametoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama na tayari IGP kwa kushirikiana na wakuu wa vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameunda kikosi kazi maalumu ili kuchunguza tukio hilo. 

Tukio la mlipuko wa bomu lilitokea juzi saa 4:30 asubuhi katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha. Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada ya uzinduzi wa Parokia. 

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Balozi wa Vatican nchini na Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Mkuu Fransisco Mantecillo Padilla.
Pia alikuwapo mwenyeji wake Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 2,000 walihudhuria ibada hiyo na tukio hilo lilitokea wakati mgeni rasmi akiwa ametoka nje ya kanisa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment