Tuesday, 7 May 2013

Upinzani wataka Jeshi la Polisi livunjwe

Dodoma. Wabunge wa Kambi ya Upinzani walicharuka bungeni jana na kuitaka Serikali kulivunja Jeshi la Polisi Tanzania na kulifanya kuwa kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwa kile walichodai kuwa limeoza na limekithiri vitendo vya dhuluma na rushwa.
Sambamba na hilo, wapinzani hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi pamoja na Mkuu wa Jeshi a Polisi nchini, Said Mwema wajiuzulu na endapo wakishindwa kufanya hivyo basi Serikali iwafukuze mara moja.
Akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani jana, Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alililaumu jeshi hilo kwa kushindwa kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyohusishwa na mambo ya udini.
“Leo kila mtu anajua taifa letu lipo katika udini, lakini Serikali inadanganya, inaingiza siasa katika mambo ‘serious’ (makini), nina hakika 
kabisa Jeshi la Polisi linamdanganya Waziri wa Mambo ya Ndani na Rais, hii ni aibu sana kwa Serikali, wananchi wanahitaji ukweli ili tu-solve tatizo (kupata suluhisho).”
“Jeshi la Polisi limeoza, ‘enough is enough’ (imetosha) tuchukue hatua, hakuna wakati wa kusubiri tena,” alisema Silinde.

Alishauri ni bora shughuli za polisi zikawa chini ya JWTZ ili kurudisha nidhamu katika jeshi hilo. Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Vincent Nyerere aliilaumu Serikali kwa kushindwa kuzuia matukio ya uhalifu.
Nyerere, ambaye ni Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), alituhumu kuwa polisi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kuvikandamiza vyama vya upinzani badala ya kulinda usalama. Alisema Kambi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini Serikali haikutoa ulinzi kwa viongozi wa dini wakati tayari ilijua kuwa ni walengwa wa mashambulizi ya kigaidi.
“Viongozi wa dini wamekuwa wakilalamika kuwa wanapokea vitisho mara nyingi lakini Serikali imekuwa haifanyi lolote,” alisema Nyerere.

Bajeti ya Wizara
Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha wa 2013/14, Dk Nchimbi alisema polisi wamekuwa na mikakati ya kupunguza uhalifu ambayo imesaidia kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu na wahalifu kwa kiwango cha juu.
Alisema Serikali inajivunia jeshi hilo kwani limefanya kazi kubwa kukabili kasi ya kutokea kwa vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, alisema pamoja na kazi nzuri ya jeshi hilo, bado wanakabiliwa na changamoto ya kudumisha nidhamu na katika mwaka uliopita wa fedha walitimua askari 99.
Dk Nchimbi alisema wizara yake imepanga kutumia jumla ya Sh741 bilioni kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh578 bilioni ni matumizi ya kawaida wakati Sh271 bilioni ni matumizi mengineyo. Mishahara itachukua Sh306 milioni.
chanzo:mwananchi

No comments:

Post a Comment