Monday, 7 October 2013

Kigoma All Stars ni mfano wa kuigwa.

WASANII wazawa wa Mkoa wa Kigoma ambao ni miongoni mwa washiriki katika Tamasha la Serengeti Fiesta, wamemwagiwa sifa kutokana na umoja wao wa kujipatia fursa kimaisha.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, katika semina ya fursa inayokwenda sambamba na tamasha hilo iliyofanyika Tanga na Moshi mwishoni mwa wiki.
Ruge alisema ni wakati wa kuthamini fursa kama ambavyo walifanya kundi la wasanii wazawa wa Kigoma wanaojiita Kigoma All Stars, ambao wanafanya vema kwa sasa katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya.
“Nimetolea mfano wa kundi hilo, kutokana na umoja wao ambao umewakutanisha ikiwa ni fursa ya wao kujipatia mambo mbalimbali ya kimaendeleo kutoka sehemu mbalimbali kama NSSF, ikiwamo mikopo, matibabu kwa kuchangia kila mwezi kiasi kisichopungua 30,000,” alisema Ruge.
Naye Meneja wa Mauzo na Masoko wa Maxi Malipo, Bernard Munubi alisema ni wakati wa Watanzania kuchangamkia fursa kupitia Tamasha la Fiesta, kwani hata kama mtu ana sh 800,000 ana uwezo wa kufanya mabadiliko kimaisha.
Semina hiyo inayowalenga vijana kuepuka kutegemea misaada kutoka serikalini, iliyohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji la Tanga na mji wa Moshi, imeishafanyika Kigoma, Tabora, Singida, Mtwara, Mbeya, Iringa, Dodoma, Morogoro, Bukoba, Shinyanga, Geita na Mwanza.
 
 

No comments:

Post a Comment