Saturday, 5 October 2013

Kitchen Party zisiwe chanzo cha kuvunja maadili.


KATIKA miaka hii kumekuwa na utaratibu usiofaa katika sherehe za Kitchen Party wa kuwahusisha mashoga.
Kutokana na utaratibu huo usiofaa kumefanya sherehe hizo kupoteza uhalisia.
Kwa tafsiri nyepesi, Kitchen Party ni sherehe ambayo hufanyika kwa lengo maalumu la kumpa vyombo vya jikoni binti anayekaribia kuingia kwenye ndoa kwa maana ya kuolewa.
Sherehe hii huambatana na mwaliko wa ndugu, jamaa na marafiki. Lakini pia huwa maalumu kwa ajili ya wanawake.
Lakini cha kushangaza hizi sherehe zimekuwa ni uwanja wa kualika wanaume wanaojifanya wanawake 'mashoga' ambao hufanya mambo ya aibu.
Mengine ni aibu kiasi cha kutotamkika, lakini ninaposikia au kuona hayo kwenye sherehe hizi huwa ninajisikia kichefu chefu.
Mashoga hawa hutumika kuonyesha mambo ambayo kimaadili hayapaswi kuonekana hadharani.
Mfano wa mambo ambayo kwa ufahamu wangu ninaona hayafai kuonekana hadharani, ni pamoja na kukata viuno hadharani, kuvua nguo na wakati mwingine hata kuonyesha namna tendo la ndoa linavyofanyika.
Wakati sisi tunakua ilikuwa ni mwiko kuona mwanamke au mwanaume akikata viuno hadharani kutokana na unyeti wa tendo lenyewe. Lakini leo hii mambo haya yamekuwa hadharani.
Hata nguo ya ndani ilikuwa haiachwi ovyo ovyo, kiasi kwamba hata unapokwenda dukani unamnong'oneza muuzaji ambaye naye huitoa kwa kificho isionekane. Lakini leo hii utamkuta mama mtu mzima mwenye maumbile makubwa  nyuma akiwa amemtanguliza shoga mbele huku anakata viuno  huku, kaning'iniza nguo za ndani nje nje bila wasiwasi.
Ninaugua juu ya hilo kwa sababu ni vitendo vya aibu ambavyo havifuati maadili ukizingatia washiriki wanaweza kuwa mama, dada au shangazi zetu hivyo suala la rika huwa halizingatiwi.
Mbali ya hayo, ninachelea kusema kuwa  mambo ambayo huonyeshwa na mashoga hao, huwa ni aibu.
Ukiangalia jinsi anavyofanya shoga na yeye ni mwanaume, ni aibu kwetu sisi wanawake kwa sababu wanaonekana ni wajuzi zaidi, hivyo wanawake huwa tunajitukanisha pasipo kujijua.
Jingine la kushangaza zaidi ni pale tunapokuwa mstari wa mbele katika kushabikia mambo ambayo hayana maana, tena kwa shangwe na vigelegele tukionyesha kufurahia mambo hayo.
Kwa upeo wangu, wakati binti anakaribia kuolewa kuna mafunzo ya ndani kabisa ambayo hupewa na bibi, shangazi au  somo ambaye ni maalumu kwa ajili ya kumfundisha namna ya kumtunza mume, usafi na kutunza familia pindi atapoingia kwenye ndoa yake.
Na baadaye sherehe za Kitchen Party hufuatia maalumu kwa ajili ya kumzawadia vyombo vya jikoni sambamba na  kuhitimisha kwa sherehe za kuagwa rasmi na familia, ndugu jamaa na marafiki.
Huo ndiyo utaratibu ninaoufahamu mimi. Lakini leo hii utaratibu huu umebadilishwa kiasi cha Kitchen Party kuwa mahali ambako hufanyika vitendo vinavyochochea vitendo vya kisagaji, ushoga, ulevi, matusi ya nguoni na wakati mwingine hata ugomvi.
Binafsi sipendezwi na hili kwakuwa lengo ni kujenga na si kubomoa. Je, kizazi kilichopo na kijacho kinajifunza nini?
Na inakuwaje kinamama watu wazima ndio wanakuwa mashabiki wa mambo yasiyo ya msingi? Je, mmerogwa au mnajitoa ufahamu? Ni lazima kuita mashoga?
Ifike mahali tuwe na hofu ya Mungu kwa kuzingatia maadili  kwa maana ya kwamba wanawake tunaweza, na hatuna haja ya kuita mashoga wanogeshe Kitchen Party ilihali si mahali sahihi kwao.
chanzo:daima.

No comments:

Post a Comment