Wednesday 16 October 2013

Walter Kanda Auawa akimwokoa baba yake

MFANYABIASHARA maarufu katika mji mdogo wa Galapo, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, Walter Kanda (31), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi alipokwenda kumuokoa baba yake, John Kanda (62), aliyevamiwa nyumbani kwake.
Katika uvamizi huo licha ya kumuua mfanyabiashara huyo, watu hao pia waliiba vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na bunduki aina ya Rifle iliyokuwa ikimilikiwa na Kanda na kutokomea nayo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda ya Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alisema uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio hilo ili kuwabaini wahusika kama hawana mahusiano na majangili wanaotafutwa.
“Tukio la mauaji ni tukio kubwa na linahitaji uchunguzi makini ili kujiridhisha na wote wanaotuhumiwa kabla ya hatua nyingine za kisheria kufuatwa kwani mbali na mauaji hayo kuna silaha imeibwa, pia kuna migogoro ya mashamba, lakini kule pia yapo matukio ya uwindaji haramu, hivyo inahitaji uchunguzi wa kina kujiridhisha,” alisema Mpwapwa.
Habari za ndani zinasema kuwa tayari kuna watu kadhaa wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo akiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Endadoshi, Kata ya Qash, Luka Bunye (CCM)  kwa tuhuma za kuhusika katika tukio hilo.
Pamoja na mwenyekiti huyo pia wapo wakulima wenzake, Everest Joachim, mkazi wa Kijiji cha Halah  na Jumanne Manja wa Qash Mwisho.
Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 8, mwaka huu, saa 5:30 usiku.
Habari zaidi zimeeleza kuwa kabla ya tukio hilo, Kanda (62), ambaye ni baba yake marehemu alitoka ndani kwenda chooni na ghafka alikutana na kundi la watu waliomrushia risasi kwa kutumia silaha inayosadikiwa kuwa ni bastola huku wengine wakimkata mapanga.
“Risasi hiyo ilipiga ukuta wa choo, nikamrukia mmoja nikawa najikinga naye ili yule mwenye bastola asinipige, tukaburuzana hadi mlango wa choo. Nikamsukumia kwa wenzake, nikapata nafasi nikaingia chooni na kufunga mlango,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kuingia chooni, watu hao walianza kusukuma mlango huku akipiga kelele za kuomba msaada, ghafla mtoto wake alitoka nje na kuwatambua wale watu ndipo walipompiga risasi ya ubavuni na kuanguka.
“Watu hao waliingia ndani na kuchukua bunduki yangu aina ya Riffle, fedha na nyaraka zinazohusu mashamba yangu, ambapo tayari majirani walikuwa wameanza kutupa mawe juu ya nyumba yangu, hivyo wakakimbia kusikojulikana,” alisisitiza.
Eneo hilo limegubikwa na migogoro ya mashamba kwa muda mrefu, inayosababisha hofu baina ya wakazi wa maeneo hayo.
chanzo:daima

No comments:

Post a Comment