MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ameendelea kuwabana vigogo wanaotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha kwenye benki za nje, akisema tayari amemwandikia Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe katika mkutano ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora jana kabla ya kuendelea na mikutano yake ya kuimarisha chama, Zitto alisema mwaka 2012 nchi ya Uswisi iliwatangaza Watanzania sita walioweka zaidi ya dola milioni 190 katika benki za nchi hiyo.
Alisema baada ya taarifa hizo, alitoa hoja bungeni, ambayo iliungwa mkono na kutakiwa kufanyika uchunguzi.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema kuwa azimio la Bunge namba sita 2012, liliitaka serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa bungeni mwezi Aprili mwaka huu, jamboaliloeleza kuwa bado halijatekelezwa hadi sasa.
Aliongeza kuwa kutokana na ukimya huo wa serikali tayari amemwandikia Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe katika Bunge la sasa.
Kwa mujibu wa Zitto, tangu Serikali ya Uswisi ilipotoa taarifa za kuwapo Watanzania sita waliohifadhi mabilioni hayo katika benki za nchi hiyo, imebainika kuwa idadi ya wanaohifadhi fedha nje imeongezeka.
Alisema kuwa sasa wamefikia Watanzania zaidi ya 200 walioweka fedha sehemu mbalimbali zinazokadiriwa kufikia dola milioni 500.
Zitto alisema hivi karibuni ataelekea Ulaya kwa ajili ya kuonana na serikali za Uswisi, Ubelgiji na Uingereza na kwamba huko atapata taarifa zaidi ya majina ya watu walioficha fedha baada ya kupata mwaliko wa nchi hizo.
“Nimealikwa Uswisi kuonana na serikali ya nchi hiyo, nitafika pia Ubelgiji na Uingereza, huko tutaongelea masuala ya utoroshaji wa fedha na naomba niwatonye, kamati iliyoundwa kuchunguza sakata hilo ina vijana wazalendo ambao wameahidi kuweka mambo hadharani kama serikali itashindwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, atapaswa kueleza sababu za vyama vinavyopokea ruzuku kutoka serikalini kushindwa kukaguliwa hesabu zao licha ya sheria kutaka vikaguliwe.
Alisema kuwa mbali na Jaji Mutungi, viongozi wengine watakaokabiliana ana kwa ana na kamati yake leo ni makatibu wakuu wa vyama vya siasa vinavyopokea ruzuku.
Zitto alisema amelazimika kuahirisha ziara yake ya ujenzi wa chama Kanda ya Magharibi kwa ajili ya kushughulikia suala hilo, aliloelezea kuwa ni muhimu katika kuonesha uwazi kwa viongozi wa kisiasa.
Alisema sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1995, kifungu cha 14, kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kinavitaka vyama vya siasa kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Aliongeza kuwa kifungu cha 18(A), kinataka vyama vikaguliwe kwa mapato ambayo vinapata kutoka vyanzo vingine.
“Nimemwita Msajili wa Vyama kwenye kamati ili kupitia mahesabu yaliyokaguliwa ya vyama vya siasa, kwa kuwa hiyo ruzuku ni kodi ya wananchi na wanapaswa kufahamishwa kodi yao inatumika vipi,” alisema.
Zitto alifafanua kuwa vyama vinavyopokea ruzuku hupatiwa jumla ya sh bilioni 20 kila mwaka
chanzo:daima
No comments:
Post a Comment