Monday 11 November 2013

Mke wangu kaniambia hawezi kumwacha wa zamani `aliyemtoa ujana` nifanyaje?

“Mimi naitwa Rajabu. Kisa changu mimi niliwahi kuoa mke wangu tukawa tunaelewana sana na kubahatika kupata mtoto mmoja wa kiume. Kabla hajajifungua akanishauri tupime Ukimwi.
“Mimi nikamuuliza ni kwanini mke wangu unaniambia tukapime HIV wakati mimi na wewe tulishapima tena ANGAZA na vyeti tunavyo kwani kuna nini huko kliniki unakokwenda mke wangu?
“Akanijibu akasema; ndiyo hivyo. Mimi nikapata alama ya kujiuliza sikupata majibu. Akaniambia mimi bwana alionitoa bikira siwezi kuachana naye. Mimi nikamuuliza, mbona sikuelewi…shida yako nini, kupima ukimwi au shida ni kurudiana na bwanako alokutoa bikira? Basi mimi nikawa sina la kufanya.
“Baada ya kunisumbua kwa muda mimi nikaamua kwenda kupima kama niko salama. Nikaenda kwa daktari na baada ya vipimo akaniambia mbona una HIV? Dah! Mimi sikulala usiku mzima. Kesho yake ikabidi nimuite mke wangu nimwambie hivi unajua mimi nina matatizo gani?
“Akasema sijui. Nikamwambia mimi nina HIV. Akaanza kulia na mimi nikamwambia unalia nini wewe ndiyo umesema huwezi kuachana na mwanaume alokutoa bikira…usilie. Akasema yule ana HIV wewe una uhakika gani kama ana HIV?
“Kufikia hapo, akaamua kuondoka kwao. Je, mimi nifanyeje amezaa mtoto ana miaka mitatu mimi nilimhudumia mpaka akajifungua mke wangu yupo kwao sasa naishi na HIV.
Kuhusu hali ya mtoto anasema; “ mpaka sasa sijui kama mzima au anaumwa kwani huyo mwanamke aliondoka naye”.
Mpenzi msomaji, nilipomuuliza kama anayo mawasiliano na mkewe huyo tokea aondoke akajibu; “ yeye huwa anakuja kwangu mara kwa mara kuniomba pesa na akija ananiuliza ulishaanza dawa? Nami huwa namwambia usiniulize. Kwa hiyo mimi nimfanyeje huyu mwanamke?” anamalizia ujumbe wake.
Mpenzi msomaji, hayo ndiyo yaliyomkuta mwenzetu na sasa anaomba ushauri. Binafsi yapo maswali ambayo najiuliza kuhusiana na kisa cha jamaa huyu.
Kwa maelezo yake, walishapima HIV kabla ya mkewe kujifungua. Kitu ambacho hakukiweka wazi ni kama baada ya kujijua kuwa ameathirika aliwahi kumshauri mkewe naye akapime kuona kama ni salama au la.
Mpenzi msomaji, mwenzetu huyu anaomba ushauri namna ya kuendeleza maisha katika hali yake hiyo. Nimemtumia ujumbe ujumbe mfupi wenye maswali kadhaa yakiwamo yafuatayo; hivi sasa anaishi wapi, ana kazi gani na baada ya kujua hali yake aliwahi kumshauri mkewe akapime na mtoto.
Haya. Mchezo ni ule ule wa watu kujidanganya kuwa chungu cha zamani ni mali. Msemo huu ulikuwa sahihi zamani wakati ambapo maisha yalikuwa rahisi yaliyojaa uaminifu tofauti na sasa tamaa zimeharibu maadili ndani ya familia zetu.
Hata kama tutasema ‘mavi ya kale hayanuki’, hakuna kitu hapo. Hivi hujui chakula kimeshatiwa mchanga? Utakulaje. Chukua hatua mapema. Magonjwa ni mengi yenye mtego, mengine hayana dawa. Sasa uking’ang’ania mchuchu wa zamani ambaye hujui kapitia njia zipi na kuamini bado ni salama, jaribu uone moto wake.
Watu yafaa kujifunza kutokana na mifano ya wengine.
Kama umeshapima na mwenzio na kukuta salama, ya nini kuibua mahusiano ya zamani? Kijana anayeomba ushauri inaonekana hata yeye mwenyewe alishangaa kuambiwa ana tatizo.
Na hofu yake kubwa inatokana na mkewe kumtamkia hadharani kuwa bado anampenda mwanaume wa awali ambaye ‘alimtoa ujana’ wake. Na kizunguzungu zaidi bado hajajua mkewe kama ni mzima au la pamoja na mwanae.
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment