FAMILIA ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu,Regia Mtema (CHADEMA), imeandaa misa takatifu ya kumbukumbu ya miaka miwili tangu afariki dunia Januari 14 mwaka 2011.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Remija Mtema alisema misa hiyo itafanyika kesho asubuhi katika Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea, Dar esSalaam na baadae familia, viongozi, wananchi na wanachama wenzake watakutana nyumbani kwake Mbezi Makabe.
“Natumia fursa hii kuwakaribisha viongozi wa CHADEMA, serikali, wanachama, marafiki na wananchi wote waliomfahamu na kumpenda Mheshimiwa Regia enzi za uhai wake, kujumuika nasi katika misa takatifu na baadae nyumbani kwake,” alisema Mtema.
Mtema alisema katika kumbukumbu hiyo, Mfuko wa Regia ulikusudia kuzindua kitabu cha kero na wasifu wake, lakini wameshindwa kufanya hivyo kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya kuandaa vitu hivyo.
Alisema watu mbalimbali katika mitandao na vyombo vya habari walipendekeza kero ambazo marehemu Regia alizikusanya kwa wananchi wake wa Jimbo la Kilombero, zitengenezewe kitabu na baadae zikabidhiwe kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda kama kumbukumbu bungeni.
Ndugu huyo alisema baada ya wazo hilo, walianzisha Mfuko wa Regia ambao ulizinduliwa mwaka mmoja baada ya kifo chake.
Alisema katika kumbukumbu hiyo ya mwaka mmoja iliyofanyika katika Hoteli ya Peakcock jijini Dar es Salaam, viongozi mbalimbali wa kisiasa, kiserikali, wanachama na wananchi walichangia mfuko huo, lakini hadi sasa ahadi hizo bado hazijatimizwa.
Aliwaomba wote walioahidi, kutimiza ahadi zao, ili waweze kutimiza malengo ya mfuko wa kutaka kuweka kumbukumbu zake na ahadi yake ya kutaka kuwasaidia walemavu na wanaoishi katika mazingira magumu.
Mtema aliwataka watakaokuwa tayari kutoa fedha walizoahidi kuwasiliana na Mwenyekiti wa Mfuko wa Regia, Santus Msimbe kwa namba 0782 820820
chanzo:tz
No comments:
Post a Comment