Siyo siri kwamba ujio wa simu za kiganjani umeongeza kasi ya ndoa nyingi kubomoka. Simu hizi baada ya kusambaa kila kona, zimerahisisha sana mawasiliano kati ya mtu mmoja na mwingine tofauti na ilivyokuwa kabla.
Huko nyuma, ukimpenda mtu, mfano umemkuta mahali, jinsi ya kumfuatilia ilikuwa ni vigumu ikilinganishwa na sasa mtu akiwa na simu yako anakupata kirahisi na hata kukutana siyo vigumu.
Na zaidi ya yote, mazungumzo mengi yanaweza kumalizwa kwenye simu.
Baba mwenye ndoa, au mama wenye ndoa, hata kama yuko na mwenzi wake karibu, simu yaweza kupigwa ikitoka kwa hawara na mazungumzo yakafanyika kwa amani pasipo upande mmoja kugundua.
Lakini kimbembe ni pale mmoja wa wanandoa anapofuma simu ya mwenzake na kuanza kudodosa nani kapiga au nani katuma ujumbe gani. Hii imeleta mitafaruku mikubwa sana kwa wanandoa.
Na wanandoa siku hizi wengi wamekuwa wakiwekeana mitego. Kwa mfano, mama anaweza kuhisi nyendo fulani fulani za mumewe, ama kwa kuambiwa au kwa kudadisi yeye mwenyewe.
Baada ya kujiridhisha anachohisi, anaweza kuvizia simu ya mumewe na kuona nani kapiga au ujumbe gani umetumwa.
Upo mfano hai niliodokezwa na dada mmoja wakati nahudhuria mkutano, akielezea jinsi anavyohisi kuwa tayari ametingisha ndoa fulani.
Alisema kuwa yupo baba mmoja mwenye ndoa yake lakini anampenda sana. Ni mtu mwenye pesa nyingi na maisha ya familia yake ni nzuri. Anasema naye(bibie) anampa ngawira(fedha) za kutosha.
Ikatokea mke wa jamaa huyo aliinasa simu ya mumewe, kudadisi akagundua namba ya simu akaipiga.
Kumbe namba ile ni ya bibie naye akapokea… halo baby..haloo baby…(wakati huo haloo zikirushwa mama yuko kimya).
Bibie kuona simu haijibiwi, akatuma ujumbe wa simu…Baby mbona huongei wakati naona kabisa umepokea? (ujumbe huo utatumwa na mama akausoma).
Baadaye baba akampigia bibie, na hii ni baada ya kupata kashkash toka kwa mkewe kuhusu simu ile iliyomwita mumewe baby na pia ujumbe wa maandishi.
Bwana huyo alichomwambia bibie ni kwamba simu ile pamoja na ujumbe vimezua mtafaruku mkubwa ambao bado haijulikani mwisho wake utakuwaje. Kisha jamaa akakata simu.
Mpenzi msomaji, njia hii ya simu imetikisa ndoa nyingi na kufifisha kabisa uaminifu ndani ya familia zetu. Japokuwa mawasiliano ni muhimu lakini changamoto ni nyingi.
CHANZO:Nipashe
Marafiki nao wamechangia mitikisiko ndani ya ndoa zetu. Wapo marafiki ambao utakuwa nao lakini siyo wema wako.
Wengine hawafurahii mfumo wa maisha unaoishi pale unapokuwa wa neema, wengine wanafanya kila wawezalo waopoe mke au mume wa mwenzake na kadhalika. Ili mradi tu wasababishe mtikisiko ndani ya ndoa husika.
Watu wakubwa japokuwa wana uwezo mkubwa wa mitaji lakini utashangaa ndoa zao zipo zipo tu.
Kila mtu analala chumba chake, kila mtu amemuachia mwenzake uhuru wa kufanya atakalo na wasisumbuane; lakini ukiwaona kwenye mikusanyiko wako pamoja ila nyumbani moto unawaka.
Wenye uwezo mkubwa wa fedha ndiyo hao wana nyumba ndogo kila kona, kisa wana fedha za kutosha. Hawa ni nadra utakuta nyumba kubwa(mke mkubwa) katulia, kwani wengi ni vurugu kila kukicha.
Wapo waliotengana kwa mama kuwafuata watoto ughaibuni na kumwacha baba akimwaya mwaya na vimwana na kadhalika. Hili ni tatizo badala ya watu kulia kivulini, amani inakuwa kitendawili.
Wapo waliopendana, wakaoana lakini hali ya kimaisha ikawa siyo nzuri. Baba familia ikamshinda akaanza kupepesa nje na kukumbana na kinamama wenye uwezo na kuwarubuni.
Je, ndoa ya awali itakuwepo? Haya, mama naye anamuona mume choka mbaya, anakumbana na kibosile mwenye vijisenti vyake, anampa mahitaji muhimu kwa kificho, je, kuna ndoa hapo?
No comments:
Post a Comment