Monday, 17 February 2014

Said Mwema, amewataka Watanzania wampokee vizuri uraiani

ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, amewataka Watanzania wampokee vizuri anapoingia uraiani baada ya kumaliza muda wake wa utumishi.
Utawala wa Mwema ulitiwa doa na matukio mbalimbali ya kihalifu, ikiwemo kutekwa, kuumizwa na kutupwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Matukio mengine ni ulipuaji wa mabomu katika mikutano ya kisiasa, kidini pamoja na kumwagiwa tindikali kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini.
Akizungumza katika sherehe za kumuaga zilizofanyika jana katika viwanja vya polisi Kurasini jijini Dar es Salaam, aliwataka Watanzania wampokee uraiani na kuahidi kushirikiana nao kulinda usalama wa nchi.

Mwema pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuongoza jeshi hilo tangu mwaka 2006.
Alisema katika kipindi chake cha kutumikia jeshi, alikutana na changamoto mbalimbali, lakini anamshukuru Mungu alizikabili na amestaafu salama.
Alibainisha kuwa alifanya kazi hiyo kwa uaminifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ndani ya jeshi hilo ambalo hivi sasa linafanya kazi kwa weledi mkubwa.
Katika sherehe hizo, Mwema alikagua gwaride la askari polisi pamoja na kupanda katika gari aliloandaliwa ili kukamilisha uongozi wake ndani ya jeshi hilo.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na mrithi wake, IGP Ernest Mangu na viongozi mbalimbali wa jeshi hilo, wakiwamo makamanda wakuu wa polisi hapa nchini.
chanzo::tz daima

No comments:

Post a Comment