Wasichana wameendelea kung’ara kwa mara nyingine tena dhidi ya wavulana baada ya kufaulu kwa asilimia 97.66 kulinganisha na wavulana waliofaulu kwa asilimia 95.25 katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Mei 2014.
Aidha, ufaulu wa jumla kwa matokeo hayo umepanda hadi kufikia wastani wa asilimia zaidi ya asilimia 90 kulinganisha na mwaka jana ambapo jumla ya watahiniwa waliofanya vizuri walikuwa ni 44,366, sawa na asilimia 87.85.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, alisema watahiniwa wote walikuwa 40,695, kati yao 1,273 hawakufanya mtihani. Katika idadi hiyo, 38,905 walifaulu.
Watahiniwa wasichana waliofaulu ni 12,080 (asilimia 97.66) huku wavulana wakiwa 26,825, sawa na asilimia 95.25 Wasichana walifanya vizuri zaidi pia katika matokeo ya mtihani huo mwaka jana, waliofaulu wakiwa 14,622, sawa na asilimia 89.19 dhidi ya wavulana 29,744, sawa na asilimia 87.21.Watahiniwa 42,952 sawa na asilimia 99.35 walifanya mtihani ambapo wasichana walikuwa ni 13,883 (99.54%) na wavulana ni 29,069 (99.27%).
Katika hatua nyingine, Dk. Msonde alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 30,225, sawa na asilimia 85.73 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu, wakiwamo wasichana 9,954 sawa na asilimia 90.59 na wavulana 20,271, sawa na asilimia 83.53.
Alisema idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 4,260 sawa na asilimia 80.73 ikilinganishwa na mwaka jana, ambao watahiniwa wa kujitegemea 4,124 sawa na asilimia 53.87 walifaulu mtihani huo.
Aidha alisema ufaulu wa masomo yote 14 ya msingi umepanda ukilinganishwa na mwaka jana. Ufaulu wa juu ukiwa ni wa somo la Kiswahili kwa asilimia 99.88 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hilo.
Ufaulu katika masomo ya sayansi (Physics, Chemistry, Biology na Advanced Mathematics) umeendelea kuimarika kulinganisha na ufaulu wa masomo hayo mwaka jana.
VIPAJI MAALUM ZACHEMSHA
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa katika shule 10 bora, ni shule moja tu inayochukua wanafunzi wenye vipaji maalum ya Kibaha ndiyo iliyopenya kwa kuwamo katika kundi hilo baada ya kushika nafasi ya tano huku nyingine za wavulana za Ilboru, Mzumbe, Tabora Boys na wasichana za Msalato na Kilakala zikikosekana.
Katika orodha hiyo ya 'top 10' iliyozingatia shule zenye idadi ya watahiniwa wasiopungua 30, sekondari ya Igowole ya Iringa ndiyo inayokamata nafasi ya kwanza na kufuatiwa na Feza Boys’ ya Dar es Salaam, Kisimiri (Arusha), Iwawa (Njombe), Kibaha (Pwani), Marian Girls (Pwani), Nangwa (Manyara), Uwata (Mbeya), Kibondo (Kigoma) na Kawawa ya Iringa.
Aidha, Dk. Msonde alizitaja shule 10 zilizo mkiani kuwa ni Ben Bella ya Unguja, Fidel Castro (Pemba), Tambaza (Dar es Salaam), Muheza High School (Tanga), Mazizini (Unguja), Ufundi Mtwara (Mtwara), Ufundi Iyunga(Mbeya), Al-Falaah Muslim (Unguja), Kaliua (Tabora) na Osward Mang’ombe ya Mara.
WANAFUNZI WALIONG'ARA
Kaimu Katibu huyo wa NECTA alisema watahiniwa waliofanya vizuri zaidi wamepatikana kwa kuangalia wastani wa alama (GPA) kwenye masomo tahasusi (combination) pamoja na wastani wa alama za jumla walizopata.
Aliwataja watahiniwa 10 bora waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi kitaifa kuwa ni Isaack Shayo (St. Joseph’s Cathedral - Dar es Salaam), Doris Atieno Noah (Marian Girls -Pwani), Innocent Yusufu (Feza Boys - Dar es Salaam), Placid Pius (Moshi - Kilimanjaro), Abubakar Juma (Mzumbe-Morogoro), Mwaminimungu Christopher (Tabora Boys -Tabora), Chigulu Japhaly (Mzumbe - Morogoro), Hussein Parpia (Al-Muntazir- Dar es Salaam) na Ramadhani Msangi wa Feza Boys ya Dar es Salaam.
Watahiniwa 10 bora waliofanya vizuri katika masomo ya biashara kitaifa ni pamoja Jovina Leonidas wa sekondari ya Nganza (Mwanza), Nestory Makendi (Kibaha - Pwani), Imma Anyandwile (Umbwe - Kilimanjaro), Theresia Marwa (Loyola - Dar es Salaam), Grace Chelele (Loyola - Dar es Salaam), Betrida Rugila (Baobab - Pwani), Jacqueline Kalinga (Weruweru- Kilimanjaro), Tajiel Kitojo wa Arusha, Shriya Ramaiya (Shaaban Robert -Dar es Salaam) na Mwanaidi Mwazema wa Weruweru Kilimanjaro.
Dk. Msonde aliongeza kuwa NECTA imezuia matokeo ya watahiniwa 150 wa shule ambao hawajalipa ada ya mitihani hadi watakapolipa huku matokeo ya watahiniwa wengine wawili yakifutwa kwa kosa la udanganyifu.
... Aliyeongoza anena
Mtahiniwa Isaack Shayo wa Shule ya St. Joseph Cathedral ya jijini Dar es Salaam ambaye amekuwa wa kwanza kwa masomo ya sayansi kitaifa amesema kuwa amestushwa na matokeo hayo kwani, ingawa aliuona mtihani kuwa ni wa kawaida hakutarajia kuwa wa kwanza.
Akizungumza na NIPASHE jana katika mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwao Mbezi Goig, Shayo alisema kuwa kusoma sana vitabu mbalimbali vya sayansi, ubora wa walimu shuleni kwao na kuhudhuria kwake masomo mengi ya ziada 'tuition' ni miongoni mwa sababu za kufanya vizuri.
“Kwakweli namshurku sana Mungu. Mtihani niliuona wa kwaida sana na hivyo kuamini kuwa ni lazima nitafaulu... lakini siyo kwa kiwango hiki. Nimefurahi sana kwa sababu najua kuwa sasa nina kazi ya kuongeza nguvu zaidi ili kutimiza ndoto yangu ya kuwa mhandisi wa majengo," alisema Shayo aliyezaliwa Dodoma mwaka 1994.
Akizungumzia maisha yake ya shule, alisema alianza darasa la kwanza katika Shule ya St. Mary mwaka 2001 na mwaka 2005 alihamia Shule ya St. Patrick darasa la sita na baadaye akamalizia darasa la saba shule ya Filbert Bay kabla kujiunga na sekondari ya Alpha.
Katika matokeo ya kidato cha nne, alisema alifaulu daraja la kwanza kwa kupata pointi 13."Nilipangiwa kidato cha tano katika Shule ya Vipaji Maalum ya Tabora Boys, lakini wazazi wangu wakanipeleka St.Joseph’s Cathedral," alisema.
Shayo alisema nje ya masomo yake anapendelea kusikiliza muziki, kuangalia filamu na pia anapenda soka, ingawa yeye siyo mchezaji na anaipenda timu ya Manchester United ya England na anampenda mchezaji Robin Van Persie 'RVP'. Anapenda pia muziki wa kizazi kipya na ni shabiki wa Joh Makini.
Chakula anachopenda ni wali samaki na kinywaji chake ni maji ya matunda.
MZAZI AFICHUA SIRI YA BINTI ALIYEONGOZA
Mzazi wa msichana Doris Atieno Noah wa Shule ya Wasichana ya St. Marian Girls, ambaye amekuwa wa pili katika masomo ya Sayansi, amesema siri ya kufaulu kwa mwanawe ni juhudi, kuwa na malengo na pia kumtanguliza Mungu katika kila jambo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, baba wa Doris aitwaye Atieno Noah, amesema kuwa siku zote, binti yake amekuwa msikivu, mwenye kuzingatia maadili ya kanisa lao la Anglikana na pia amekuwa akijituma sana katika masomo kwa nia ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi wa umeme.
Na kwa sababu hiyo, Noah anasema Doris amekuwa akifanya vizuri kila anakopita na hivyo, hata matokeo yake ya sasa hayamshangazi sana.
"Labda kitu kipya kwake ni huku kuwa wa kwanza... lakini kwa ujumla familia yangu yote tumekuwa tukijua kuwa ana uwezo mkubwa sana darasani," anasema Noah, ambaye pia ana watoto wengine wanaosoma darasa la kwanza na la saba.
"Ninachoshukuru ni kwamba siku zote amekuwa mtoto mwema. Ni msikivu na daima amekuwa akipenda sana somo la mathematics (hisabati) kwa sababu anaamini kuwa ni kwa kufaulu vizuri somo hilo ndipo atakapoweza kutimiza ndoto yake ya kuwa injinia wa umeme," anasema Noah.
"Hata katika mitihani yake ya kidato cha nne alifanya vizuri sana na kuwamo katika orodha ya wasichana kumi bora kitaifa... alichaguliwa kwenda katika shule ya vipaji maalum ya Msalato (Dodoma). Hata hivyo, tukaamua kumpeleka St. Marian (Bagamoyo) kwa kuamini kuwa huko kutamsaidia kutimiza malengo yake.
"Alipomaliza kidato cha nne na kufaulu kwa alama A katika masomo yote ya Sayansi, nilijaribu kumshauri achukue mchepuo wa PCB. Hata hivyo, alinikatalia kwa kusema kuwa angeweza kufanya hivyo, lakini asichotaka ni kusoma mchepuo usiokuwa na somo analolipenda sana la Mathematics.
Hivyo akabaki kusoma PCM (Fizikia, Kemia na Hisababati) na sisi tukaendelea kumuunga mkono ili aendeleze ndoto zake za kuona kuwa siku moja anakuwa injinia mzuri wa umeme," anasema Noah.
"Sasa tunashukuru kuona kuwa amefanya vizuri sana... shukrani kwa jitihada zake, shukrani kwa walimu wake na kubwa zaidi, shukrani kwa Mungu," anaongeza Noah, mfanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambaye pia hujishughulisha na kilimo cha alizeti.
chanzo:nipashe
No comments:
Post a Comment