Tuesday, 18 November 2014

Eti vivazi mlegezo, chanzo ni baba na mama?

Haya mavazi yameharibu familia sana na baba na mama ndio chanzo kikubwa. Wakiwa kwenye mtoko (outing), mama anatinga na suruali la kubana, baba naye anatinga suruali safi ila nyuma mlegezo/mtepeto na watoto pia wanavalishwa nguo kama zao na kuwanyoa kiduku. Wa kulaumiwa hapa ni nani? Wazazi wachafuzi wa mavazi  jamani acheni hizo tabia!

Nikianza na hilo la suruali mlegezo, nakumbuka mwaka 1994 wakati wa ziara ya kimasomo Marekani, moja ya sehemu niliyobahatika kutembelea ni chuo kikuu cha Michigan State University.

Mabasi ya abiria(hapa tunaita daladala) ambayo niliona yakipita barabarani, ubavuni yalikuwa na picha mbalimbali za vijana waliokuwa wamevalia suruali mlegezo huku nguo za ndani za kila rangi zikionekana.

Nilipozungumza na baadhi ya vijana pale chuoni kuhusu picha zile waliniambia ilikuwa ni kampeni ya kupiga marufuku mavazi ya mlegezo/mtepeto kwa vijana wote wa jimbo lile. Ni takriban miaka 20 tokea wakati huo wenzetu walipiga marufuku kivazi hicho.


Hapa kwetu ndio kwanza vijana na wengine watu wazima wanalegeza utadhani ni mashindano ya kupewa medani. Kumbe wenzetu waanzilishi walishaona athari zake za kimaadili na kuachana nazo.

Msomaji mwenzetu hapo juu amejaribu kutoa mfano wa familia ambayo kuanzia wazazi hadi watoto wamejiingiza katika mkumbo huo. Hebu tujiulize, mtoto mdogo unayemvalisha suruali au kaptula mlegezo, huku akiona baba yake na mama wakivaa vivyo hivyo, huyu utamkatazaje kuendelea kupenda kivazi hicho wakati wazazi nao wamo?

Lipo jambo moja ambalo wengi wetu huwa tunalisahau au pengine ni kutokana na kutokujua maana au umuhimu wake. ASILI ZETU. Hii ikimaanisha chimbuko la kule tulikotoka au tulikoanzia.

Asili yako ni pale ulikotokea. Kwa mzazi anaweza kuwa amezaliwa kijijini au mjini. Hapo anaweza kwa namna fulani kuita ni asili yake. Mtoto aliyezaliwa mjini hujikuta akielea katika mazingira aliyoyakuta.

Kile anachokiona wazazi wake wakimfanyia ndicho anachokua nacho. Mazingira anayokulia ndiyo yanayomtambulisha kule aendako. Baba wakiwa wagomvi hata baadhi ya watoto huiga tabia hiyo siku za usoni wakijua kuwa ni kawaida. Kisa ni kutokana tu na kule kuwaona wazazi wao wakigombana.

Mzazi akiwa mlevi wa pombe au sigara, mara nyingi huchomoza watoto au mtoto katika familia ile ambaye hujikuta katika asili hiyo. Ndiyo maana mzazi anatakiwa kuwa mfano wa matendo mema anapolea watoto wake ili kuwaepusha tabia mbaya mbele ya jamii katika maisha yao baadaye.

Hata wahenga wetu walilijua hilo na kuweka wazi kuwa “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Mtoto unamnyoa kiduku(yaani ananyolewa upande wa kushoto na kulia kisha nywele zinaachwa eneo la kati kuanzia paji la uso hadi kichogoni). Anaonekana kituko kabisa mfano wa ndege fulani.

Mtoto huyu tayari anaona hiyo ni fasheni inayomtambulisha na utashangaa hata akinyolewa tofauti atalia hadi arejeshewe ile staili yake. Huku ni kumharibu mtoto kutokana na kuiga vitu ambavyo havijengi maadili bali kubomoa.

Na huyu mzazi anayevaa mlegezo mbele ya watoto sijui anakuwa na maana gani.  Sidhani kama ni mfano wa kuigwa kitabia, naye ameharibikiwa. Watu wabadilike.

Kibaya zaidi, vipo vivazi vya kinamama hasa wadada ambao wakati mwingine vinawatesa sana. Utaona mtu anataka kukaa, suruali imembana na kwa nyuma maungoni viwalo vya ndani nje! Nje!

Amevalia sketi au gauni lakini fupi hadi juu ya magoti akitaka kukaa ndio shughuli. Yaani kiguo hicho hupanda juu zaidi na kumsababishia ahangaike kukirudisha chini kwa kukilazimisha. Kumbe kiguo chenyewe kinalalamika kuwa kinataka kupanda juu zaidi. Ni kichekesho kitupu msomaji wangu.

Ukimuona mtu wa aina hii anavyohangaika kushusha au kuivuta nguo ile irefuke wakati yenyewe haitaki, unaweza kucheka sana. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo! Kumbe nisemeje basi? 

Kwanini uvae nguo ya kukunyima raha usivae ukajiachia? Aliyezoea vivazi vya aina hii atasema ni fasheni lakini fasheni inayokutesa mbele za watu, fasheni gani hiyo? Mimi ni mchokonozi tu, lakini wasemaji wapo!
chanzo:nipashe

No comments:

Post a Comment